Latest Posts

RAIS SAMIA: KITUO CHA BIASHARA UBUNGO KUONGEZA MAPATO NA AJIRA KWA VIJANA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa uzinduzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (East Africa Commercial and Logistics Centre – EACLC) ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuongeza mapato ya serikali, ajira kwa vijana, na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Akizungumza tarehe 1 Agosti 2025, wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kilichopo Ubungo, Dar es Salaam, Rais Samia amesema mradi huo unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya biashara na usafirishaji, hasa kwa kuchochea mauzo ya nje na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

Amebainisha kuwa kituo hicho kitafanya kazi kama kitovu cha biashara na usafirishaji kwa nchi zote za Afrika Mashariki kwa kuwaunganisha wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na walaji kutoka ndani na nje ya Tanzania. Eneo hilo lina maghala ya kisasa, ofisi za biashara, na huduma zote muhimu za usafirishaji zilizo katika sehemu moja, hatua itakayopunguza kwa kiasi kikubwa gharama na muda wa kusafirisha mizigo.

Rais Samia pia ameeleza kuwa mradi huo unaendana na mkakati wa serikali wa kujenga uchumi wa kidijitali, kwani shughuli nyingi katika kituo hicho zitasimamiwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kielektroniki.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya maendeleo iliyofanyika katika Jimbo la Ubungo, hususan kwenye sekta za afya, elimu, maji na miundombinu.

Prof. Mkumbo amesema kuwa tangu mwaka 2020 hadi sasa, jimbo hilo limepata mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Aidha Prof. Kitila ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo anayemaliza muda wake, ameipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Kimara Mavurunza-Bonyokwa hadi Segerea, ambayo imekuwa kilio cha wananchi kwa zaidi ya miaka 14 tangu ilipoahidiwa mwaka 2010.

“Miaka 14 tumejitahidi kupiga maneno lakini Mheshimiwa Rais mwaka 2023 uliamua barabara hii iingie katika bajeti, na mwaka wa jana Disemba ukatoa bilion 3.6, mkandarasi akaingia uwandani kwa mara ya kwanza katika miaka 14 tangu iahidiwe”, ameeleza Prof. Kitila.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameeleza kuwa idadi ya biashara katika Jimbo la Ubungo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 100, kutoka biashara 4,220 mwaka 2020 hadi 8,997 mwaka 2025 katika mitaa 46 ya jimbo hilo akieleza kuwa hiyo ni dalili tosha kuwa mazingira ya biashara yameboreshwa na uwekezaji umeongezeka kwa kasi katika mkoa wa Dar es Salaam.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!