Wamarekani watatu waliohukumiwa kifo kwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mwaka jana wamebadilishiwa hukumu zao na sasa wanatumikia kifungo cha maisha jela. Taarifa hiyo imetolewa na ofisi ya rais wa DRC.
Watatu hao walikuwa miongoni mwa watu 37 waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi mwezi Septemba mwaka jana. Walidaiwa kuhusika na mashambulizi katika ikulu ya rais na nyumba ya mshirika wa Rais Félix Tshisekedi mwezi Mei 2024.
Uamuzi wa kubadilisha hukumu zao unakuja kabla ya ziara ya mshauri mpya wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika, Massad Boulos, ambaye ni baba mkwe wa Tiffany Trump, binti wa Rais wa Marekani, Donald Trump. Boulos anatarajiwa kuwasili Kinshasa siku ya Alhamisi, kabla ya kuendelea na ziara yake nchini Rwanda, Kenya na Uganda.
Ingawa Marekani haijatangaza hadharani kuwa watatu hao wamefungwa kimakosa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilithibitisha kuwepo kwa mazungumzo baina ya nchi hizo kuhusu kesi hiyo.
Watatu hao- Marcel Malanga Malu, Tylor Thomson na Zalman Polun Benjamin walihukumiwa kwa makosa ya njama ya uhalifu, ugaidi, na mashitaka mengine, ambayo walikanusha. Kiongozi mkuu wa njama hiyo, Christian Malanga, raia wa Marekani mwenye asili ya Congo, aliuawa wakati wa shambulio hilo, pamoja na wengine watano.
Kwa jumla, watu 51 walihukumiwa katika mahakama ya kijeshi, huku kesi hiyo ikirushwa moja kwa moja kwenye televisheni na redio za kitaifa. Kati yao, 14 waliachiliwa baada ya kuthibitika kuwa hawakuwa na uhusiano na shambulio hilo.
Hukumu za kifo hazijatekelezwa DRC kwa zaidi ya miongo miwili, na badala yake, wafungwa wanaopokea adhabu hiyo hutumikia kifungo cha maisha gerezani. Rais Tshisekedi ametia saini amri ya kubadilisha hukumu hizo siku ya Jumanne, msemaji wake Tina Salama alitangaza kwenye televisheni.
Mmoja wa mawakili wa Marcel Malanga, Ckiness Ciamba, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika kesi hiyo.