Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amemshutumu rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila kwa kuunga mkono muungano wa makundi ya waasi uliowekewa vikwazo na Marekani.
Kulingana na shirika la habari la AP, Tshisekedi ametoa shutuma hizo wakati wa mahojiano na kituo binfasi cha redio siku ya Jumanne ambapo amenukuliwa akisema kwamba Kabila alisusia uchaguzi na anapanga kuanzisha uasi kwa sababu anaunga mkono muungano huo wa makundi ya waasi unaojulikana kama AFC.
Muungano huo unadaiwa kuwa vuguvugu la kisiasa na kijeshi ulioanzishwa mwezi Disemba kwa lengo la kuyaunganisha makundi yote yenye silaha, vyama vya siasa na asasi za kiraia dhidi ya serikali ya Kongo. Hata hivyo kiongozi huyo wa Kongo hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai yake.
Shutuma hizo za Tshisekedi zinafuatia tangazo la Marekani la kuuwekea vikwazo muungano wa AFC mwezi uliopita. Washington inaushutumu muungano huo kwa kujaribu kuipindua serikali ya Kongo na kuchochea mzozo mashariki mwa nchi.
Ilisema mwanachama mkuu wa muungano huo, kundi maarufu la waasi la M23 tayari liko chini ya vikwazo vya Marekani.
Tshisekedi, pamoja na wataalamu wa Marekani na Umoja wa Mataifa, wanaishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kutoa uungaji mkono wa kijeshi kwa M23. Rwanda inakanusha madai hayo, lakini mwezi Februari ilikiri vyema kwamba ina wanajeshi na mifumo ya makombora mashariki mwa Kongo ili kulinda usalama wake.