Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, amewakemea vikali mawaziri wake kwa tabia ya kusinzia wakati wa mikutano, akisema ni dalili ya kutokuwa makini, ukosefu wa nidhamu, na kutojiheshimu.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumuapisha waziri mpya, Rais Hichilema ameeleza kushangazwa na baadhi ya mawaziri wanaoshindwa kuwa makini wakati wa vikao muhimu vya serikali.
“Katika baraza la mawaziri mtu analala saa 10, swali ni walikuwa wapi… kama unaweza kuanza kudanganya huko? Kwangu mimi huo ni uhalifu, uhalifu mbaya,” amesema Rais Hichilema.
Licha ya kutofafanua moja kwa moja, vyombo vya habari vya Zambia vimetafsiri kauli yake kuwa ni onyo dhidi ya mawaziri wanaojihusisha na unynywaji wa pombe kupita kiasi na karamu za usiku.
Rais amesisitiza kuwa tabia hiyo inahatarisha siri za serikali na kuchelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Nimeshauri baraza la mawaziri kwamba lazima tujihusishe. Unapokuwa katika ofisi ya umma lazima uwe na nidhamu, sio kujifurahisha kupita kiasi,” ameongeza.
Akirejelea maandiko ya Biblia, Hichilema amesema ukosefu wa nidhamu unaweza kuangamiza maisha ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla, “Kwa hiyo unashiriki vipi katika mkutano unapolala? Ujumbe uko wazi kabisa: hupendi mashauri ya baraza la mawaziri kwa niaba ya Wazambia. Kwa hivyo kwa nini unakaa hapo?”.