Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, amewataka wafanyabiashara ndogondogo mkoani humo kutumia vitambulisho vya kisasa vya wafanyabiashara ili kujiimarisha kiuchumi kwa kunufaika na huduma zinazotolewa na taasisi za kifedha nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo, Andengenye amesema vitambulisho hivyo vimeundwa kwa teknolojia ya kisasa na vina uwezo wa kurahisisha miamala ya kifedha.
Katika awamu ya kwanza ya ugawaji, jumla ya vitambulisho 1,453 vimegawiwa kwa wafanyabiashara kutoka Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Kigoma. Vitambulisho hivyo, ambavyo vimeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), vinatarajiwa kutumika kwa kipindi cha miaka mitatu.
Andengenye amewaasa viongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanaendeleza zoezi la usajili wa wafanyabiashara na kuwahamasisha kujiandikisha kwa wakati ili kila mfanyabiashara mdogo aweze kunufaika na mfumo huo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kibiashara, sambamba na kuimarisha miundombinu muhimu inayowezesha wafanyabiashara wa ngazi zote kufanikisha malengo yao. Amesema kuwa mfumo huo ni sehemu ya jitihada za serikali za kurasimisha biashara ndogondogo na kuboresha maisha ya wananchi.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mkoani Kigoma, Mwajuma Ali, ameeleza kuwa mpaka kufikia Desemba 2024, mkoa umefanikiwa kusajili jumla ya wafanyabiashara 2,578. Lengo ni kusajili zaidi ya wafanyabiashara 5,500 ifikapo Juni 2025. Amewahimiza wafanyabiashara kuendelea kujisajili kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo, akisisitiza kuwa mfumo huo utawasaidia kuimarisha biashara zao.
Baadhi ya wafanyabiashara waliopokea vitambulisho hivyo, akiwemo John Mbuwa wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, wamesema kuwa utaratibu huo ni hatua muhimu kwa wajasiriamali wadogo kwani umewapa fursa ya kurasimisha shughuli zao na kuongeza uhuru wa kufanya biashara.
Andengenye ameendelea kusisitiza kuwa vitambulisho hivi vya kisasa ni nyenzo muhimu ya kufanikisha maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na kwa mkoa mzima wa Kigoma.