Na Josea Sinkala, Mbeya.
Timu ya madaktari bingwa 49 katika idara mbalimbali kutoka maeneo tofauti hapa nchini wamefika mkoani Mbeya na kuanzisha kambi maalum kwa ajili ya kutoa matibabu kwa wananchi katika maeneo ya jirani na makazi yao.
Akizungumza na madaktari hao, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt. Juma Homera, amesema lengo la Serikali ni kuona wananchi wote wanapata huduma za afya hasa wale wanaokabiliwa na ukosefu wa uchumi imara au kukabiliwa na magonjwa yanayohitaji waende hospitali za mbali.
Dkt. Homera amesema hiyo ni dhamira njema ya Mhe. Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza kuona wananchi wake wanahudumiwa ipasavyo ikiwemo kwenye eneo la afya hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika hospitali za Serikali hass ngazi za kuanzia kwenye wilaya zao ili kupata matibabu ya magonjwa mbalimbali ambayo yanaonekana kuwa sugu ikiwemo matatizo ya watoto, mifupa, masikio, koo, upasuaji na matatizo yahusuyo huduma za afya ya mama na mtoto.
Afisa kutoka wizara ya afya Desteria Nanyanga, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kile alichosema inajali wananchi wake hasa wasio na uwezo wa kumudu gharama za kufuata huduma za kiafya maeneo ya mbali kutokana na hali ngumu za kiuchumi.
Amesema madaktari hao wapo tayari kufanya kazi kwa weledi kuhakikisha wananchi wenye matatizo mbalimbali ya kiafya wanahudumiwa.
Baadhi ya madaktari hao wakiwemo kutoka mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Mbeya, wamewataka wananchi kufika kwenye hospitali zilizo karibu na maeneo yao hasa wilayani wakisema wako tayari kwa utoaji huduma kwa wananchi hasa katika siku sita zilizoanza Mei 26 hadi Mei 31, 2025 katika hospitali za wilaya na Halmashauri za mkoa wa Mbeya..