Na Josea Sinkala, Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera, ameongoza kikao cha baraza la ushauri mkoa (RCC) ambacho kilikuwa na agenda moja ya kupokea mapendekezo ya ugawaji na ubadilishaji majina ya majimbo katika mkoa huo.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya, amepokea taarifa hizo kutoka Halmashauri zote za mkoa huo.
Akifungua kikao hicho Mhe. Homera, amesema baada ya makubaliano ofisi yake itaandika muhtasari na kuupeleka tume ya uchaguzi ili kusubiri majibu juu ya maombi yaliyotolewa na kuridhiwa na vikao mbalimbali vikiwemo vya ushauri wilaya DCC na vile vya mabaraza ya waheshimiwa madiwani.
Wajumbe mbalimbali wa kikao cha RCC mkoa wa Mbeya kutoka wilaya za mkoa huo wameeleza kuwa ni muhimu majimbo yaliyokidhi vigezo na kulingana na jiografia ya jimbo husika yakagawanywa ili kusogeza huduma kwa wananchi.
Akizungumza kwenye hitimisho la kikao hicho, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM mkoa wa Mbeya Christopher Uhagile, amewashukuru wadau wa kikao hicho cha ushauri mkoa kwa mawazo na ushirikiano wao katika kusogeza mbele huduma za wananchi na kwamba Serikali itaendelea kuzingatia maoni ya wananchi na kwamba maendeleo hayana chama hivyo kuwaomba kuendelea kushirikiana kuujenga mkoa huo katika nyanja mbalimbali hasa kiuchumi, kijamii na kisiasa.