Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amefuturisha watoto zaidi ya 300 wanaoishi katika mazingira hatarishi ndani ya mkoa huo , huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuwapatia stadi za maisha ili kuwasaidia kujikimu na kuondokana na hali hiyo.
Katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tarehe 12 Machi 2025, Mhe. Mtanda amesema kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mpango wa kuwajengea uwezo watoto na vijana, ili waweze kupata ujuzi wa fani mbalimbali kupitia vyuo vya mafunzo stadi vya VETA.
“Nataka kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuhangaika na watoto wa mtaani kwani tukiwaacha kundi kubwa hivi ni kupoteza nguvu kazi ya taifa ambayo madhara yake ni makubwa kwa siku za usoni.”
Pia, Mtanda ametoa wito kwa maafisa ustawi wa jamii wa mkoa huo kuendelea kuwafikia wahitaji, ili kuwasaidia kuepuka kuingia kwenye shughuli hatarishi kama vile kutumia dawa za kulevya.