Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Daniel Chongolo, ameshiriki maadhimisho ya siku ya familia ya Polisi (Police Family Day) yaliyofanyika tarehe 07 Machi 2025 katika uwanja wa CCM Vwawa Wilayani Mbozi mkoani humo.
Maadhimisho hayo yameambatana sambamba na utoaji wa vyeti na tuzo kwa maofisa wa Jeshi la Polisi waliofanya vizuri kwa kujituma, kuzingatia nidhamu na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Chongolo amekabidhi zawadi kwa waliofanya vizuri ambapo hafla hiyo imehusisha michezo mbalimbali ikiwemo ngoma za asili, mpira wa miguu, mchezo wa pool table na burudani kutoka kwa waimbaji mbalimbali.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, mkuu wa mkoa wa Songwe Mhe. Daniel Godfrey Chongolo, amewapongeza maofisa wa Polisi katika mkoa wake (Songwe), wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa SACP Agustino Senga, kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kudumisha usalama, utulivu na usalama wa mkoa kwa wananchi na mali zao katika kuendelea kuendesha maisha yao.
“Kwanza, nianze kwa kuwapongeza sana kwa kutekeleza jukumu hili muhimu la kuadhimisha siku ya familia ya Askari ndani ya Mkoa wa Songwe. Hili ni jambo muhimu sana, kwani Jeshi la Polisi limepewa dhamana kubwa ya kulinda raia na mali zao. Kwa kweli, mnatekeleza jukumu hili kwa umahiri mkubwa”, ameeleza Mhe. Chongolo.
Aidha ameongeza kuwa, “Ukitaka kupima kiwango cha kazi mnayoifanya ndani ya mkoa wetu na mikoa mingine nchini, nafasi hii niliyopewa ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama Mkoa inanipa fursa ya kuwapongeza sana ninyi na askari wote wa jeshi la Polisi kwa kazi kubwa mnayoifanya kuhakikisha mkoa wa Songwe unakuwa salama na tulivu. Hongereni sana!”, amesisitiza Chongolo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe SACP Agustino Senga, amesema kuwa Jeshi la Polisi Tanzania lina utamaduni wa kuadhimisha siku ya familia ya Polisi kila mwaka ili kuimarisha mahusiano kati ya askari na jamii wanayoihudumia.
Ameeleza kuwa kwa Mkoa wa Songwe, maadhimisho hayo yamehusisha shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi katika hospitali na masoko, kutoa elimu mashuleni na kupinga vitendo vya ukatili.
Pia, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za usalama kama Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Jeshi la Wananchi, askari wa kike walitembelea watoto yatima na kutoa misaada katika hospitali na shule, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo yaliyoenda sambamba na siku ya mwanamke Duniani ambapo madhimisho ya siku ya familia kwa askari Polisi (Police Family Day) yameadhimishwa yakiwa na kaulimbiu ‘Ni wajibu wa Jeshi la Polisi kushirikiana na jamii ili kutokomeza uhalifu’.