Mradi wa kuboresha utalii kusini (REGROW) umeboresha huduma za malazi zenye jumla ya vitanda 409 katika Hifadhi za Mikumi (116) na Nyerere (120) kwa lengo la kuvutia utalii wa ndani lakini pia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limeendea kuboresha huduma za malazi katika Hifadhi za Taifa.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la Mhe. Innocent Edward Kalogeris aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani kuhamasisha Watanzania kutembelea Hifadhi zetu na kuongeza mapato ya utalii badala ya kutegemea Watalii toka nje ya Nchi.
Mhe. Kitandula alisema kuwa Serikali imeendelea kujenga huduma za malazi za gharama nafuu katika maeneo yenye vivutio vya utalii nchini ili kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani.
Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa katika kuhamasisha na kukuza utalii wa ndani, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau wa utalii imeendelea kuandaa na kushiriki kampeni, maonesho na matukio mbalimbali ikiwemo: “Twenzetu Kileleni” na “Funga Mwaka Kijanja, Talii”.
Vilevile, Wizara imeshiriki maonesho mbalimbali ya kitaifa kama vile Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Maonesho ya Wakulima Nanenane, Monesho ya Kili Fair, Maonesho ya Karibu Kusini, Serengeti Marathon, Kili Marathon, Ruaha Marathon, Simiyu Cultural and Tourism Festival, Nyangumi Festival, Kizimkazi Festival, Valentine Gateway na TANAPA, Shangwe la Sikukuu na TANAPA, Selous Marathon, Kilombero Festival na Mafia Festival ambayo yamechagiza ongezeko la watalii wa ndani.