Rais wa Kenya, William Ruto, ameweka wazi sababu zilizopelekea kufutwa kazi kwa aliyekuwa Naibu Rais wake, Rigathi Gachagua, akisema kuwa mgogoro huo ulitokana na mvutano wa ndani ya muungano wa Kenya Kwanza.
Akizungumza katika mahojiano na vituo vya redio vya lugha za kiasili Jumatatu, Ruto ameeleza kuwa mvutano huo ulianza mara tu baada ya kuingia madarakani, huku Gachagua akitofautiana na watu wake wa karibu kama mwanablogu Dennis Itumbi, wabunge Ndindi Nyoro na Kimani Ichung’wah.
“Niliuliza, ‘Kwa nini unapigana na Itumbi, PA wangu Farouk, na hawa vijana wa Mlima Kenya? Kuna haja gani ya mapambano madogo kama haya?’” Ruto amesema.
Kwa mujibu wa Rais, mtazamo wa Gachagua wa ugomvi uliwafanya wabunge kumgeuka, jambo lililomgharimu nafasi yake.
“Wabunge waliambiwa kuwa wasiponyenyekea, watarudishwa nyumbani. Kwa hivyo, waliamua kuchukua hatua kwanza,” Ruto ameeleza.
Rais huyo amesisitiza kuwa hakushiriki moja kwa moja katika kuondolewa kwa Gachagua na kwamba mchakato ulifuata sharia, huku akifichua kuwa Gachagua aliomba Ksh.10 bilioni ili kumpigia debe katika ukanda wa Mlima Kenya.
“Niliambiwa, ‘Naweza kukufanya kuwa Rais wa muhula mmoja kama hutanipa Ksh.10 bilioni za kupanga siasa za eneo hili.’ Nikakataa. Kama ni hatima yangu kuwa Rais wa muhula mmoja, iwe hivyo,” Ruto alisema.
Rais pia alipuuza hofu ya migawanyiko ya kisiasa kuelekea ziara yake ya kaunti tisa za Mlima Kenya, akisema lengo lake ni kuwapa wananchi mrejesho wa maendeleo ya serikali yake.
“Nipo hapa kwa sababu nilichaguliwa na wananchi wa Kenya, wakiwemo wa Mlima Kenya. Kuanzia kesho (Jumanne), itakuwa wazi kama nimetimiza ahadi zangu,” alisema.
Akijibu ukosoaji kutoka kwa Gachagua na wandani wake, Ruto alitetea rekodi yake ya maendeleo kwa kutaja miradi ya miundombinu iliyotekelezwa chini ya uongozi wake.
“Nimesikia baadhi ya viongozi wakisema sijafanya lolote. Lakini mimi ndiye niliyefanikisha ujenzi wa barabara kutoka Marua kupitia Wamunyoro, ambako mkosoaji huyo anaishi,” alisema kwa kejeli inayoonekana kumlenga Gachagua.