Rais wa Kenya William Ruto amewataka wazazi kuwajibika zaidi katika malezi ya watoto wao, akisisitiza kuwa jukumu hilo haliwezi kuachwa kwa serikali wala taasisi za kidini.
Akihutubia waumini wa Kanisa la AIC Bomani, Kaunti ya Machakos, Jumapili, Ruto alisema watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu na lazima waelekezwe na kulelewa na familia zao.
“Watoto wetu ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa familia na taifa. Malezi ni jukumu la kipekee kutoka kwa Mungu. Msiviachie kanisa wala serikali,” alisema Ruto. “Msiruhusu watoto wenu kulelewa na wapita njia.”
Rais aliwahimiza wazazi kutowatelekeza watoto wao hadi wafikishwe kwa polisi, akieleza kuwa vyombo vya dola haviwezi kuwa suluhisho la upungufu wa malezi nyumbani.
“Polisi wamefundishwa kukabiliana na wahalifu, si kulea watoto. Ukimwachia mtoto wako polisi, unatarajia nini?” alisema Rais Ruto. “Mimi hujipanga kulea watoto wangu, na kila mzazi anapaswa kufanya hivyo.”
Ruto pia alilaani kile alichokitaja kuwa matumizi mabaya ya vijana na baadhi ya viongozi wa kisiasa katika maandamano ya kupinga serikali, akisema ni uongozi wa hovyo kutumia watoto wa taifa kwa misingi ya kisiasa.
“Viongozi, tuache kuwapotosha watoto wetu kwa kuwachochea waingie mitaani kufanya fujo na kuharibu mali,” alisema. “Kama mpango wako wa kisiasa ni kusubiri ghasia ili upate nafasi ya kujitokeza kisiasa, basi huo ni uongozi wa kiwango cha chini kabisa.”
Rais alihimiza mshikamano wa kitaifa ili kuelekeza nguvu, vipaji na elimu ya vijana katika ujenzi wa taifa badala ya vurugu na migawanyiko.
“Nguvu na vipaji vya vijana ni rasilimali muhimu katika ujenzi wa Kenya. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwaongoza, kuwalea na kuwahamasisha ili watoe mchango wao kwa njia chanya.”
Kauli ya Ruto imekuja wiki moja baada ya kutoa agizo la “kupiga risasi mguuni” wale wote watakaokamatwa wakiharibu mali za watu au kuvamia vituo vya polisi.
“Mtu yeyote anayevamia biashara ya mwingine, kituo cha polisi au anachoma mali za watu, apigwe risasi mguuni na akalazwe hospitalini kabla ya kufikishwa kortini,” alisema Ruto jijini Nairobi Julai 9. “Kama ni kuadhibu, adhibiwe kisawasawa kwa mujibu wa sheria.”
Rais alisisitiza kuwa shambulizi dhidi ya vituo vya polisi ni kitendo cha kigaidi, akisema serikali yake haitakubali taifa litawaliwe kwa fujo na vitisho.
“Kuna watu wanashambulia vituo vya polisi, hiyo ni tangazo la vita. Hii ni ugaidi na tutakabiliana nalo kwa nguvu zote.”
Matamshi ya Rais yanakuja wakati maandamano yanazidi kushika kasi kote nchini Kenya, yakichochewa na hasira ya umma dhidi ya gharama ya juu ya maisha, ukandamizaji wa wapinzani na matumizi ya nguvu ya polisi dhidi ya waandamanaji.
Kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR), maandamano ya Julai 7 yalisababishavifo vya watu 31 na majeruhi 107. Wakati huohuo, maandamano ya Juni 25 yaliyopinga Mswada wa Fedha wa 2024 yaliripotiwa kuua watu 16, wengi wao kwa risasi za polisi, kulingana na ripoti ya Amnesty International Kenya.
Maeneo kadhaa pia yameripoti visa vya uporaji wa mali, kuharibiwa kwa biashara na misururu ya visa vya ukamataji kiholela, huku kukiwa na madai ya uporaji unaofadhiliwa kisiasa.