Latest Posts

SADC YAAMUA KUONDOA VIKOSI VYAKE DRC, YATILIA MKAZO MAZUNGUMZO YA KISIASA

Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamefanya uamuzi wa kumaliza rasmi operesheni ya kijeshi ya SAMIDRC iliyokuwa imepelekwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Uamuzi huu unamaanisha kuwa vikosi vya SADC Mission in the Democratic Republic of Congo (SAMIDRC), vilivyotumwa Desemba 2023, vitaanza kuondolewa kwa awamu kutoka DRC.

Baada ya mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya mtandao siku ya Alhamisi, taarifa ya viongozi wa SADC iliyotolewa ilisema kuwa mzozo wa DRC unapaswa kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia na kisiasa, huku wakitambua ongezeko la mahitaji ya kibinadamu katika eneo hilo.

“Mkutano umemaliza rasmi mamlaka ya SAMIDRC na kuelekeza kuanza kwa uondoaji wa awamu wa wanajeshi wa SAMIDRC kutoka DRC,” taarifa hiyo imesema.

Mkutano huu umefanyika baada ya vikosi vya waasi wa M23 kuchukua udhibiti wa mji wa Goma mwezi Januari, hali iliyosababisha vifo vya angalau wanajeshi 20 kutoka Afrika Kusini, Tanzania, na Malawi waliokuwa sehemu ya operesheni ya SAMIDRC.

Licha ya kujitahidi kwa mwaka mmoja kupambana na waasi wa M23, operesheni ya SAMIDRC haikuleta mafanikio yaliyotarajiwa. Katika taarifa yao, viongozi wa SADC walisema:

“Mkutano umesisitiza kujitolea kwake kwa kushughulikia mzozo unaoendelea DRC na kuahidi kuunga mkono juhudi za kurejesha amani na usalama katika eneo hilo, kulingana na Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa SADC wa mwaka 2003.”

Wamesema pia walihofia hali inayoendelea kuzorota mashariki mwa DRC, ikiwa ni pamoja na kutekwa kwa miji muhimu kama Goma na Bunagana, pamoja na kufungwa kwa njia kuu za usambazaji misaada ya kibinadamu.

Hata hivyo, viongozi hao wamewasifu wanajeshi wa SAMIDRC kwa kujitoa mhanga, mshikamano na uthabiti wao katika operesheni hiyo tangu mwanzo wake.

Mnamo Januari, Rais wa Rwanda Paul Kagame alilaani operesheni ya SAMIDRC, akisema kuwa haikuwa kikosi cha kulinda amani bali ni jeshi linalopendelea upande wa serikali ya DRC.

Kagame pia aliionya Afrika Kusini, ambayo ni kati ya nchi zilizotoa wanajeshi wengi kwa SAMIDRC, akisema kwamba ikiwa inataka mgongano na Rwanda, basi itakabiliana nayo ipasavyo.

Licha ya shinikizo la kimataifa na vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Kigali, Rwanda imeendelea kukanusha madai ya kuisaidia waasi wa M23.

SADC sasa imeelekeza juhudi zake katika mchakato wa kisiasa, ikihimiza ushirikiano wa pamoja kati ya jumuiya za SADC na Afrika Mashariki (EAC) ili kuunganisha mazungumzo ya Luanda na Nairobi kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kudumu. Taarifa hiyo iliongeza kuwa:

“Mkutano umesisitiza haja ya suluhisho la kisiasa na kidiplomasia linalojumuisha wadau wote, wakiwemo mataifa, makundi ya kijeshi na yasiyo ya kijeshi, kwa lengo la kurejesha amani na utulivu mashariki mwa DRC.”

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!