Latest Posts

SAFARI YA MAFANIKIO YA NHC NA MIAKA MINNE YA UONGOZI WA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

Na Mwandishi Wetu,

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuwa chachu ya mageuzi makubwa katika sekta ya nyumba nchini Tanzania, likitimiza jukumu lake la kipekee la kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1962 kwa Sheria ya Bunge Na. 45, Shirika limeendelea kusimamia maono ya waasisi wa Taifa, likiongozwa na dira ya maendeleo endelevu ya makazi. Hata hivyo, miaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta kasi mpya na mafanikio makubwa yanayostahili kusimuliwa.

Historia na Maono ya Kuanzishwa kwa NHC

Shirika hili liliundwa kama sehemu ya maono ya Mwalimu Julius Nyerere ya kuhakikisha mahitaji ya msingi ya mwanadamu yanapatikana kwa urahisi. Katika miaka ya mwanzo, NHC lilitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya umma, lakini changamoto za kiuchumi na kisheria zilianza kuathiri utendaji wake.

Mageuzi ya kihistoria yalifanyika katika miaka ya 1990 hadi 2008, ambapo sheria zisizokuwa rafiki katika maendeleo ya sekta ya nyumba zilibadilishwa, na NHC likapewa mamlaka mapya ya kujiendesha kibiashara bila kusahau jukumu lake la msingi. Hatua hizi ziliweka msingi wa kuboresha huduma za makazi kwa Watanzania, lakini ni katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia ambapo kasi ya utekelezaji wa miradi ya nyumba imeongezeka kwa kiwango cha kipekee.

Mageuzi na Mpango Mkakati wa Maendeleo

Mwaka 2015, NHC lilianzisha Mpango Mkakati wa Miaka 10 (2015/16 – 2024/25), uliolenga kujenga nyumba 10,000 na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi. Lakini ni katika kipindi cha Uongozi wa Dkt. Samia ambapo utekelezaji wa mpango huu umechukua sura mpya, ikiwemo uanzishaji wa miradi mikubwa kama “Samia Housing Scheme” ambayo inatarajiwa kuwa zitajengwa nyumba 5,000 katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Mafanikio Makubwa Katika Sekta ya Nyumba

Ujenzi wa Nyumba za Makazi na Biashara

Hadi sasa, NHC limefanikiwa Kujenga zaidi ya nyumba 30,000 za makazi tangu kuanzishwa kwake na linaendelea kujenga nyumba za kuuza na kupangishwa.

Katika kipindi cha Awamu ya Sita, NHC imekamilisha miradi mikubwa ya nyumba za makazi kama vile:Nyumba 887 za makazi katika eneo la  Iyumbu na Chamwino, Dodoma.

Mradi huu umejengwa eneo la Iyumbu (303) na Chamwino(101) Jijini Dodoma, nyumba nyingine mpya 68 ujenzi unaendelea eneo la Iyumbu na umefikia 90%  na ujenzi wa nyumba 521 za makazi na biashara zimejengwa katika maeneo ya Mtukula-Kagera; Medeli-Dodoma na Dar es Salaam.

Ukamilishaji wa miradi mikubwa ya Kawe 711 na Morocco Square

Shirika katika kipindi hiki cha Awamu ya Sita, lilipanga kukamilisha miradi mikubwa iliyokuwa imesimama tangu mwaka 2018. Baada ya kuingia madarakani, Mheshimiwa Rais aliikwamua miradi hii kwa kuliruhusu Shirika la Nyumba la Taifa kukopa hela za kuikamilisha miradi hii.

Morocco Square

Katika kipindi cha miaka minne ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Shirika limefanikiwa kukamilisha mradi wa Morocco Square kwa 100%. Shirika linaendelea kuuza na kupangisha ambapo maeneo ya maduka (Retail Mall) yamepangishwa kwa asilimia 100 na Ofisi asilimia 95 imepangishwa. Katika jengo lenye nyumba za makazi 100, tayari nyumba 85 zimeshauzwa na mauzo ya nyumba zilizobakia yanaendelea. Aidha, upangishaji wa Hoteli yenye vyumba 81 umefanyika kwa asilimia 100 na hoteli hiyo imeanza kutoa huduma.

Kawe 711

Mkandarasi Estim Construction Company Limited alirejea katika mradi Januari 2024  na ujenzi wa mradi wa nyumba 422 pamoja na sehemu za biashara unaendelea katika mradi wa Kawe 711. Mradi huu una thamani ya Shilingi Bilioni 169. Ujenzi umefikia asilimia 50. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2026

Miradi wa “Samia Housing Scheme”

Ili kuenzi kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani, na ili akumbukwe katika sekta ya nyumba, Shirika lilibuni mradi wa nyumba 5000 wa Samia Housing Scheme. Mradi huu umeleta matumaini mapya kwa wananchi. Katika eneo la Kawe, Dar es Salaam, ujenzi wa nyumba 560 ulianza na umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Februari 2025. Mradi huu utawezesha ujenzi wa nyumba 5,000 katika maeneo mbalimbali nchini zenye gharama ya shilingi bilioni 466. Mauzo ya nyumba 560 eneo la Kawe hizo yamekamilika na NHC inajiandaa kuanza awamu ya pili ya mradi huu eneo la Kawe (560) na Mdeli Dodoma (100).

Kwa ujumla, miradi ya Kawe 711 na Morocco Square inaenda kuboresha mandhari ya miji na kukuza uchumi wa Tanzania.

Utekelezaji wa ujenzi wa majengo ya kimkakati ya shughuli za Ofisi na biashara

Kahama – Utekelezaji wa mradi huu umefikia 70% na unatarajiwa kukamilika Januari 2025.

Masasi Plaza – Masasi Mtwara – Ujenzi wa jengo la biashara katika mji wa Masasi upo 40%.

Mtanda Lindi- Ujenzi wa jengo la biashara Mtanda Commercial Building-Lindi umefikia 30%.

2H Commercial Building – Morogoro – Ujenzi wa jengo hili la biashara umefikia 40%.

 

Usanifu na Usimamizi wa Miradi ya Ujenzi

Katika kipindi hiki, Shirika ni msimamizi na mshauri Elekezi wa miradi kadhaa ifuatayo:-

a) Usimamizi wa ujenzi soko la Kariakoo wenye thamani ya shilingi bilioni 28 umekamilika na ujenzi umefikia wastani wa asilimia 97. Mradi huu ulitarajiwa kukamilika Januari 2025

b) ) Usanifu na Usimamizi wa jengo la Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango eneo la Mtumba umekamilika na ujenzi umefikia asilimia 85 na Mjenzi ni Kampuni ya Estim Construction;

c) Usimamizi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira Awamu ya Pili ujenzi umefikia asilimia 88 na Mjenzi ni Suma JKT;

d) Usanifu na ujenzi wa jengo la soko la madini (Tanzanite) eneo la Mirerani Manyara – Usanifu umekamilika na ujenzi umefikia asilimia 86.

 

Utekelezaji wa sera ya ubia

Baada ya kuingia madarakani Dkt Samia Suluhu Hassan alifungua milango ya uwekezaji nchini na akahimiza ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma ili kuharakisha ujenzi wa uchumi wa Tanzania. Shirika la Nyumba la Taifa ili kuenda sambamba na maono ya Mheshimiwa Rais, liliiboresha sera yake ya ubia na ikazinduliwa na Waziri Mkuu Novemba 16, 2022. Mwaka 2024, Shirika liliidhinisha na kusaini mikataba ya miradi 21 ya ubia yenye thamani ya TZS 179 bilioni. Kwa sasa Miradi 18 iliyopata vibali vya ujenzi imeanza kutekelezwa na ujenzi wake upo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine 3 imeshapata vibali hivi karibuni na itaanza kutekelezwa.

Aidha, Shirika limeendelea kusimamia miradi ya ubia ya sasa na ya zamani iliyokuwa imesimama ambayo ipo maeneo mbalimbali nchini. Miradi minne iliyokuwa imesimama imesharejeshwa kwenye Shirika ili ikamilishwe na Shirika lenyewe. Lengo la Shirika ni kuhakikisha miradi yote ya ubia isiyokamilika inarejeshwa katika Shirika na mazungumzo na wabia wenye miradi hiyo yanaendelea.

Kadhalika, Shirika linaendelea na mchakato wa upembuzi na tathimini ya kina kwa waombaji wapya kwa miradi mingine kwenye maneneo kadhaa yanayohitaji kuendelezwa na sasa iko kwenye hatua ya kupata idhini kwa ajili ya kuendeleza  viwanja hivyo visivyopungua 80 kwa nchi nzima.

Kupitia sera ya ubia, NHC limefanikiwa kushirikiana na sekta binafsi kujenga majengo ya kisasa ya makazi na biashara na kupendezesha mandhari ya miji yetu. Eneo la Kariakoo pekee lililokuwa na wapangaji 172 ambao nyumba zao zimevunjwa na kuendelezwa, sasa zitapatikana nyumba Zaidi ya 2100 za makazi na biashara. Haya ni mageuzi makubwa sana.

Utekelezaji wa Miradi ya Ukandarasi

Katika kipindi cha Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, NHC ilipewa miradi kadhaa ya kimkakati ya ukandarasi yenye thamani ya TZS Bilioni 186 ambayo imekamilika au ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji eneo la Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma. Ujenzi wa majengo ya Ofisi nane za Wizara umefikia asilimia 90.

Miradi mingine iliyotekelezwa na NHC katika Awamu hii ni pamoja na Ujenzi wa jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (umefikia asilimia 80) na ni mradi unaogharimu TZS 9.7 Bilioni. Aidha, NHC inajenga jengo la Tanzanite huko Mererani, Manyara (asilimia 86), Ujenzi wa Hospitali za Kanda ya Kusini (Mitengo) na Hospitali ya Kanda ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Musoma, Mara ambayo imekamilka na ukamilishaji wa Jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete ambayo nayo imekamilika kwa asilimia 100. Ujenzi wa jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha UDSM umekamilika kwa asilimia 80. Miradi mingine ni ujenzi wa jengo la Ofisi pamoja na uzio wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Temeke Dar Es Salaam umefikia asilimia 40 na ujenzi wa ghala la chakula la Halmashauri ya Masasi Vijijini ambao umekamilika kwa asilimia 100.

Kadhalika, katika kipindi hiki, Shirika lilikamilisha pia ujenzi wa miradi 17 yenye majrengo 44 ya Wakala wa Misitu Tanzania-TFS yenye thamani ya shilingi Bilioni 12.96. Aidha majengo mawili ikiwemo Ofisi na miundombinu kwa ajili ya tanuru (incinerator) la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamilika kwa asilimia 100 Jijini Dodoma. Aidha,ujenzi wa mradi wa jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dodoma unaendelea na umefikia asilimia 34.

Matengenezo ya nyumba za Shirika

Katika kipindi hiki, Shirika lilikamilisha ukarabati wa majengo katika mikoa mbalimbali ya Shirika ambayo ulijumuisha kupaka rangi na ujenzi wa mifumo ya maji taka.  Tangu mwaka 2023 Shirika limekuwa likitenga shilingi bilioni 7 kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zake nchini kote. Hii imewezekana kutokana na kuimarika kwa uwekezaji na mapato ya Shirika.

Ukuaji wa pato la Shirika

Kutokana na ukuaji wa Shirika uliowezeshwa na sera imara za Serikali ya Awamu ya Sita, ankara za kodi ya nyumba zimepanda kutoka shilingi bilioni 7.5 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 9.4 hivi sasa, huku makusanyo ya kodi hiyo yakiwa zaidi ya asilimia 100. Vilevile, Mwaka 2021 Shirika lilikuwa na maeneo yasiyopangishwa (vacancies) yanayofikia nyumba 700 na sasa maeneo hayo yameshapangishwa kwa asilimia 80, hii ikitokana na kuimarika kwa uchumi na biashara za watanzania.

Shirika limefanikiwa kukusanya madeni yake ambapo katika kipindi hiki Shillingi bilioni 8.3 zimekusanywa.  Aidha, kutokana na kuimarika kwa vipato vya wananchi wakiwemo wapangaji, mauzo ya nyumba mpya yameongezeka ambapo kwa mradi wa Kawe pekee wenye nyumba 560, nyumba zote zimeshauzwa hata kabla mradi haujakamilika.

Thamani ya Rasilimali za Shirika yaimarika

Rasilimali za Shirika hadi kufikia Juni 2024 kwa hesabu zilizokaguliwa na CAG zimefikia  5.47 Trilioni ikilinganishwa na mwaka 2021 ambao zilikuwa TZS 5.04 Trillion. Ukuaji huu  unatokana na kuongezeka kwa milki za Shirika kutokana na kukamilika nyumba mpya na umiliki wa maeneo mbalimbali ikiwemo Shirika kufanikiwa kununua ardhi na majengo katika eneo la Urafiki, Dar es Salaam, ambayo awali yalikuwa yakimilikiwa na Kampuni ya Tanzania-China Friendship Textile Mills Co. Mnada wa kuuzwa eneo hili uliendeshwa na Kampuni ya Udalali ya Santana Investment Limited na NHC kufanikiwa kununua ekari 105 za ardhi katika viwanja vitatu vya kimkakati Jijini Dar es Salaam. Licha ya uwepo wa unit 399 kwa ajili ya makazi pia kuna majengo ya biashara 6, makazi ya wataalamu 32, Shule ya msingi, retail shop 32, maghala 31, yadi za magari 10, gereji 4, kituo cha mafuta 1, sehemu za kuosha magari 3, fremu ndogo ndogo, makontena na Industrial park.

Ushirikiano na Sekta ya Fedha

Kupitia ushirikiano na benki zaidi ya 22, NHC limewezesha wananchi kupata mikopo ya nyumba ya muda mrefu. Aidha, sera ya ubia iliyohuishwa mwaka 2022 imefungua milango kwa sekta binafsi kushiriki katika miradi ya nyumba yenye thamani ya shilingi bilioni 191.

 

Miradi inayoanza kutekekezwa hivi karibuni

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa mafanikio makubwa, huku hatua mbalimbali za utekelezaji zikiwa zimefikiwa.

Miradi inayokaribia kuanza hivi karibuni  ni Singida 2F uliopo Singida, Kashozi Business Center, Bukoba Mjini, Samia Housing Scheme Kawe Awamu ya 2 na Kijichi Jijini Dar es Salaam. Miradi mingine ni Mt. Meru Plaza eneo la Kibla Jijini Arusha, Juwata Plaza Morogoro, Medeli Awamu ya 3 Dodoma, Mkwakwani Plaza Tanga na Tabora Commercial complex.

Miradi mingine ni Iringa ICC, Mpwapwa Flats Dodoma, Ilala Breweries Retail Shops na Mtwara Warehouse.

 

Mustakabali wa NHC

NHC linaendelea kupanua wigo wa shughuli zake kwa kutumia teknolojia za kisasa na utaalamu wa ndani. Katika miaka ijayo, Shirika linatarajia kuendelea kufanya yafuatayo:

Kuanzisha miradi mipya ya makazi, Kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), kutekeleza miradi ya ukandarasi, ujenzi wa vitega uchumi, Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa miradi mbalimbali nchini na kutekeleza sera ya ubia.

 

Hitimisho

Kwa miaka minne ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, NHC limepiga hatua kubwa katika kuboresha sekta ya nyumba nchini. Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha kila mmoja anapata haki ya makazi bora. Kwa mipango madhubuti, NHC itaendelea kuwa mwanga wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!