Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kilichopo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kimetumia Shilingi bilioni 40 kujenga bwawa la maji lenye uwezo wa ujazo wa lita milioni 3.5, litakalosaidia kumwagilia hekta 800 za mashamba ya miwa ndani ya kipindi kisichopungua miezi minane.
Mradi huo ambao chanzo chake kikuu cha maji ni Mto Wami unalenga kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika kiwanda hicho, hususan wakati wa kiangazi, ili kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinaendelea mwaka mzima.

Akizungumza wakati wa ziara ya wahariri waliotembelea kiwanda hicho, Mhandisi Joel Saimon amesema mpango uliopo ni kuunganisha mabwawa mawili ili kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa mwaka mzima.
Amesema kukamilika kwa maboresho hayo kutakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha shughuli za uzalishaji wa sukari kiwandani hapo, pamoja na kuhakikisha mashamba ya miwa yanapata maji ya kutosha.

Kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi, Aron Mwaigaga, ameeleza namna kiwanda hicho kinavyotekeleza shughuli za uzalishaji wa sukari, hatua za uzalishaji pamoja na shughuli mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana.
Naye Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Idrisa Lungiro, amesema ziara hiyo imempa fursa ya kujifunza na kupata uelewa zaidi kuhusu uwekezaji, teknolojia na shughuli za uzalishaji zinazofanyika katika kiwanda hicho.
