Latest Posts

WANAOISHI NA VVU WATAHADHARISHWA KUTOKUACHA MATUMIZI YA DAWA ZA ARV.

 

Wito umetolewa kwa watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kuzingatia matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza virusi hivyo (ARV), baada ya kubainika kuwa baadhi yao huacha kutumia dawa hizo, hali inayoweza kuhatarisha afya zao.

Akizungumza katika uzinduzi wa zoezi la upimaji wa VVU kuelekea maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Iringa, Dkt. Godfrey Mtunzi, amesema baadhi ya sababu zinazochangia watu kuacha kutumia dawa hizo ni pamoja na uoga, aibu, matumizi ya tiba mbadala pamoja na imani za kidini.

Dkt. Mtunzi ameeleza kuwa kuacha kutumia dawa za ARV kunaweza kusababisha virusi vya UKIMWI kupata usugu dhidi ya dawa, hali inayoweza kupunguza ufanisi wa matibabu na kumlazimu mgonjwa kubadilishiwa aina nyingine za dawa.

Awali akihutubia wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, amesema kati ya wananchi 27,346 walijitokeza kupima VVU mwaka huu, wananchi 356 walibainika kuwa na maambukizi huku watu 16,397 tayari wanatumia dawa za kufubaza virusi hivyo.

Akizungumzia zoezi hilo, Mratibu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Kanda ya Kati, Yeriko Kawanga, amewahimiza wananchi wa Iringa kujitokeza kupima VVU ili kujua hali zao za kiafya na kuwataka wale watakaobainika kuwa na maambukizi kuanza matibabu mapema.

Kawanga amesisitiza kuwa matumizi ya dawa za ARV ni muhimu kwa watu wanaoishi na VVU, akieleza kuwa kutotumia dawa hizo kunaweza kusababisha afya kudhoofika na kuongeza hatari ya madhara yatokanayo na maambukizi hayo.

Zoezi la upimaji wa VVU na utoaji wa elimu linafanyika katika vituo tisa vilivyopo kwenye kata sita za Manispaa ya Iringa, likitarajiwa kuhitimishwa Desemba Mosi, siku ambayo huadhimishwa kama Siku ya UKIMWI Duniani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!