Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni, amewaonya baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Same wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vinavyosababisha migogoro katika maeneo yao, akiwataka kuzingatia misingi ya utawala bora, kuheshimu mamlaka na kutambua mipaka ya majukumu yao ili kuimarisha ushirikiano katika kusimamia maendeleo ya wananchi.

Ametoa onyo hilo katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Same, akieleza kuwa baadhi ya madiwani wamekuwa wakionesha mwenendo wa kutotii maelekezo halali ya viongozi, kudharau mamlaka na kuingilia mipaka ya kiutendaji, hali inayochangia kuibuka kwa migogoro baina yao, watendaji wa kata na wenyeviti wa vijiji, jambo linaloweza kudhoofisha utendaji wa serikali za mitaa na huduma kwa wananchi.
Mgeni amesema uongozi ni dhamana inayohitaji nidhamu, heshima, ushirikiano na uwajibikaji, hivyo diwani anapaswa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za wananchi badala ya kuchochea tofauti na migawanyiko.

Ameonya kuwa diwani yeyote atakayebainika kukiuka sheria, kanuni na taratibu za uongozi atachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Aidha, amewataka madiwani kutekeleza wajibu wao kwa karibu zaidi na wananchi, ikiwemo kufuatilia miradi ya maendeleo, kusikiliza kero na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza katika kata zao, akisisitiza kuwa si sahihi kusubiri ziara za viongozi wa ngazi ya wilaya ndipo matatizo ya wananchi yaanze kushughulikiwa, kwani uwajibikaji wa viongozi unapaswa kuonekana katika utendaji wa kila siku.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bw. Rashid Jasper, amesisitiza umuhimu wa madiwani kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao na kutatua tofauti zinazojitokeza kwa kuzingatia taratibu za kiuongozi, akieleza kuwa mshikamano baina ya viongozi ni muhimu katika kuhakikisha halmashauri inatimiza wajibu wake na kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi.
Naye Katibu wa Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Bw. Mohamed Ifanda, amesema chama hakitavumilia madiwani watakaokiuka taratibu za uongozi na kushindwa kutekeleza wajibu wao, akionya kuwa hatua zitachukuliwa kwa watakaobainika kutowajibika, ikiwemo kutoshiriki katika ziara za viongozi wa ngazi ya wilaya wanapofika katika kata zao bila sababu za msingi, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi kutanguliza maslahi ya wananchi kuliko tofauti binafsi.
