Latest Posts

TANZANIA YAONGEZA KASI UTEKELEZAJI WA AZIMIO LA KAMPALA (CAADP)

 

Tanzania imeeleza dhamira ya kuongeza kasi ya mageuzi katika Sekta ya Kilimo kwa kuimarisha utekelezaji wa Azimio la Kampala chini ya Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Kilimo Barani Afrika (CAADP), unaolenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kukuza ajira na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Akizungumza Novemba 20, 2026, jijini Dodoma, wakati wa kuhitimisha Ziara ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Azimio la Kampala iliyofanyika katika Hoteli ya Best Western, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Athumani Kilundumya, amesema azimio hilo linaendana na vipaumbele vya Serikali katika kuleta mageuzi ya kilimo kupitia sera, mikakati na uwekezaji wenye lengo la kuongeza tija na ushindani wa mazao ya kilimo.

Mhandisi Kilundumya, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerald Mweli, amesema ziara hiyo imeongeza uelewa kwa wadau kuhusu malengo ya Azimio la Kampala na kutoa nafasi ya kujadili mikakati ya kuharakisha mageuzi ya kilimo, ikiwemo kuongeza uzalishaji, kukuza biashara ya mazao na kuimarisha viwanda vinavyotegemea malighafi za kilimo.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Sekretarieti ya SADC, Serikali ya Sudan Kusini, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, katika kuhakikisha ajenda ya CAADP inatekelezwa kwa kuimarisha uwekezaji katika umwagiliaji, matumizi ya teknolojia za kisasa, huduma za ugani na upatikanaji wa masoko.

Aidha, amesisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kujenga mifumo imara ya uzalishaji wa chakula na lishe, kuongeza fursa za ajira kwa vijana na wanawake pamoja na kuimarisha uwezo wa sekta ya kilimo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Azimio la Kampala linatoa mwelekeo wa pamoja kwa nchi za Afrika kuharakisha mageuzi ya kilimo kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha usalama wa chakula kupitia mifumo endelevu ya uzalishaji.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!