Latest Posts

TIBA YA WANYAMA WANAWAKE WAPIGA HATUA

Taaluma ya tiba ya wanyama nchini Tanzania imeendelea kushuhudia ongezeko la ushiriki wa wanawake, tofauti na miaka ya awali ambapo idadi yao ilikuwa ndogo, huku wataalamu hao wakitakiwa kuongeza mchango wao katika kukabiliana na magonjwa yanayoathiri wanyama na yale yanayoweza kuambukizwa kwa binadamu.

Hayo yameelezwa katika Kongamano la 43 la Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA), lililofanyika mkoani Morogoro na kuwakutanisha wadau wa sekta ya wanyama na mifugo, likiambatana na maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya tiba ya wanyama nchini huku Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kikitajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuandaa wataalamu wa sekta hiyo.

Akizungumzia changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele katika sekta hiyo, Dkt. Julius Keyu, Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), amesema mwingiliano kati ya binadamu, mifugo na wanyamapori ni miongoni mwa changamoto kubwa kutokana na uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa kati ya makundi hayo.

Akifafanua mchango wa mafunzo ya tiba ya wanyama katika kukabiliana na changamoto hizo, Peter Msola, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na mwanzilishi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama, amesema tangu kuanzishwa kwa mafunzo hayo mwaka 1976, jumla ya madaktari wa wanyama 1,583 wamehitimu, wakiwemo wanawake 226 sawa na asilimia 14.4.

Kwa upande wake, Doreen Ndosi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambaye pia ni mjumbe wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania, amesema katika kipindi cha miaka 50 wanawake wamepiga hatua kubwa katika taaluma hiyo, jambo linaloonesha mabadiliko ya ushiriki wao na umuhimu wa kuendelea kuwapa nafasi zaidi katika sekta hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!