
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kung’ara katika ujenzi na utoaji wa nyumba bora kwa Watanzania, huku likifikia mafanikio makubwa kupitia miradi yake ya kimkakati ikiwemo Samia Housing Scheme, ambapo nyumba zote 560 zimeshachukuliwa kabla ya kukamilika rasmi.
Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam leo Juni 16, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah Hamad, amesema mafanikio haya ni matokeo ya usimamizi madhubuti, ubunifu wa miradi ya kisasa na jitihada za dhati za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika maelezo yake, Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa mbali na mafanikio ya Samia Housing Scheme, NHC pia imefanikiwa kufufua mradi wa Kawe 711 uliosimama kwa miaka minane na sasa unaendelea kwa kasi kubwa, sambamba na miradi mingine ikiwemo GPR na Morocco Square ambayo sasa imejaa wapangaji katika nyumba za makazi, hoteli na ofisi.
“NHC sasa imepunguza deni lake kutoka shilingi bilioni 27 hadi bilioni 22 baada ya kukusanya bilioni 5 kwa kushirikiana na taasisi za serikali. Pia tumefanikisha ukarabati wa nyumba 3,004 katika majengo 205, huku nyumba 1,546 zikiwa bado zinaendelea kukarabatiwa,” alisema Hamad.
Vilevile amesema, NHC inaendelea kutekeleza sera ya ubia kwa mafanikio makubwa ambapo miradi 21 yenye thamani ya shilingi bilioni 351 inaendelea katika mikoa mbalimbali na miradi mingine 64 ya thamani ya bilioni 607 iko kwenye hatua ya tathmini ya wawekezaji.
Katika kuhakikisha ustawi wa jamii, NHC pia limechangia kiasi cha shilingi Bilioni 1.42 kwa miaka mitano iliyopita kupitia sera yake ya huduma kwa jamii (CSR), huku likijikita pia katika kampeni kabambe ya ukusanyaji wa kodi na madeni kwa kushirikiana na taasisi kama NIDA, BRELA na Msajili wa Hazina.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amepongeza juhudi za NHC kwa kuikwamua miradi iliyokwama, akiitaja NHC kama chombo muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa makazi bora nchini, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ina upungufu wa nyumba milioni 3.8.
“Majengo ya NHC yamegeuka kuwa mapambo ya Jiji la Dar es Salaam. Juhudi hizi zinaokoa maisha ya Watanzania wengi wanaohitaji makazi bora. NHC mnayo nafasi kubwa katika kulijenga taifa letu,” alisema Balile.
Katika hatua nyingine, Shirika hilo linatarajia kuanzisha NYUMBANI BOND, mpango mpya wa uwekezaji utakao wawezesha Watanzania kununua hisa na kusaidia kuongeza mtaji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba zaidi nchini.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linabakia kuwa taasisi kinara katika ujenzi wa taifa kupitia makazi bora, ya kisasa na yanayokidhi mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi.