Latest Posts

SAMWEL (20) ATUHUMIWA KUMUUA MPENZIWE WA MIAKA 52, MKOANI MARA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Samweli Emmanuel (20), maarufu kwa jina la ‘Nzaliya’, mkazi wa kijiji cha Nata, Wilaya ya Serengeti, kwa tuhuma za mauaji ya kikatili ya Josephina Magani (52), ambaye alikuwa akiishi naye kama mpenzi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Jeshi hilo, tukio hilo la kusikitisha lilitokea usiku wa Mei 7, 2025, majira ya saa 1:00, katika kitongoji cha Mambaswe, kijiji cha Nata. Inadaiwa kuwa Samweli alimshambulia Josephina kwa kutumia kisu na kumchoma tumboni, na kusababisha upotevu mkubwa wa damu uliosababisha kifo chake papo hapo.

Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa anadaiwa kuburuta mwili wa marehemu kutoka nyumbani kwake na kuupeleka kwenye shimo lililotumika awali kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu, na kuuficha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia, ambapo mtuhumiwa alimshutumu marehemu kwa madai ya kumuambukiza virusi vya UKIMWI.

“Tunatoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za matukio ya uhalifu kwa wakati,” amesema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara.

Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza umuhimu wa amani na maelewano katika jamii na familia, na kueleza kuwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!