Latest Posts

SEKONDARI JITEGEMEE JKT KUFANYIWA UKARABATI KWA LENGO LA KUONGEZA UFAULU

Uongozi wa Shule ya Sekondari Jitegemee JKT iliyopo jijini Dar es Salaam umetangaza kuwa upo kwenye mkakati wa kuboresha miundombinu ya shule hiyo, ikiwemo kuondoa majengo chakavu, ili kuboresha mazingira ya kujifunza na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Petro Ngata, wakati wa mahafali ya 40 ya kidato cha nne ya shule hiyo.

Ngata amesema ukarabati huo utahusisha kuboresha madarasa, maabara, na miundombinu mingine ya shule kwa ushirikiano kati ya uongozi wa shule na Shirika la JKT, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunza.

“Tunataka Shule yetu ya Jitegemee JKT iwe na muonekano mpya, hivyo kila mmoja wetu ana wajibu wa kuchangia maendeleo haya kwa kushiriki katika ukarabati huu,” alisema Ngata.

Aidha, Ngata alisema kuwa wanaendelea na jitihada za kukusanya fedha kwa ajili ya ukarabati huo, huku wakilenga pia kuboresha ufaulu wa wanafunzi kupitia maboresho katika mfumo wa kufundisha na kujifunza.

Ngata pia aliwasihi wahitimu wa kidato cha nne kuacha fikra za kutafuta maisha nje ya nchi na badala yake watumie rasilimali zilizopo nchini kuongeza pato la taifa. Alisisitiza kwamba mataifa ya nje yanavutiwa na rasilimali ambazo Tanzania imejaaliwa kuwa nazo, hivyo vijana wanapaswa kuzitumia kwa maendeleo ya nchi.

“Msitamani kwenda nje ya nchi, kwani wengine wanatamani kuja hapa kutumia rasilimali zetu. Mungu ametubariki na rasilimali ambazo hazipatikani kwingineko, hivyo tumieni maarifa mliyopata kuzitumia ipasavyo,” aliongeza.

Naye Mkuu wa Shule hiyo, Kanali Robert Kesi, alieleza kuwa wanafunzi wameandaliwa vyema kwa kufanya mitihani ya majaribio yenye viwango vya kitaifa, kwa nadharia na vitendo, na wameiva tayari kwa mitihani yao rasmi.

Awali, akisoma risala ya wahitimu, Shekha Said alibainisha kuwa moja ya mafanikio waliyoyapata ni kujifunza elimu ya ujasiriamali, ambapo wanaweza kutengeneza sabuni, kilimo cha mbogamboga, na kutengeneza balbu zilizoharibika. Wahitimu 89 waliagwa rasmi shuleni hapo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!