


Viongozi wa Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa wamesema kuwa, Uwanja wa Ndege wa Iringa ni fursa muhimu kwa wananchi wa Iringa vijijini na taifa kwa ujumla, hasa katika kukuza utalii, biashara, na uchumi wa kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi hao leo Machi 14, 2025, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya iringa vijijini Anorld Mvamba
amesema kuwa, uwanja huo umefungua milango kwa watalii wa ndani na nje kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na vivutio vingine vilivyopo Iringa vijijini kwa urahisi.
“Iringa ni kitovu cha utalii, na uwanja wa ndege huu umesaidia kupunguza muda wa safari kwa wageni. Hii inatoa nafasi kwa hoteli, waongoza watalii, na wafanyabiashara wa sekta hiyo kunufaika zaidi,” alisema.
Aidha, Mvamba amesema kuwa uwanja huo umeongeza fursa za biashara kwa wakulima na wafanyabiashara wa Iringa vijijini kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao kama mahindi, viazi, alizeti, na chai kwenda masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Uwepo wa usafiri wa anga unasaidia kuongeza thamani ya mazao yetu kwa kuyafikisha sokoni kwa haraka, jambo linalowanufaisha wakulima na wafanyabiashara wa Iringa,” alisisitiza.
Katika sekta ya uchukuzi, amesema uwanja huo umekuwa mkombozi kwa wafanyabiashara, wawekezaji, na watumishi wa umma kwa kurahisisha safari za kikazi , hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Pia, amebainisha kuwa uwanja wa ndege huo umeongeza fursa za ajira kwa vijana na wanawake wa Iringa kupitia biashara za usafiri wa teksi, huduma za hoteli, na kazi nyingine zinazohusiana na uwanja wa ndege.
“Hili ni jambo kubwa kwa wananchi wetu, hususan vijana na wanawake, ambao sasa wanaweza kujikita katika biashara na huduma zinazotokana na ukuaji wa sekta ya anga,” alisema Mvamba.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wa Sekretarieti ya CCM Wilaya ya Iringa Vijijini wamewahimiza wananchi kutumia fursa ya usafiri wa anga kwa safari zao, kwani kwa sasa kuna ndege za moja kwa moja kati ya Iringa na Dar es Salaam kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATC). Wamesema usafiri huo ni wa haraka, salama, na wa gharama nafuu ukilinganishwa na muda na gharama zinazotumika kusafiri kwa barabara.
“Wananchi wa Iringa Vijijini wanapaswa kuchangamkia huduma hii ili kurahisisha shughuli zao za kibiashara, utalii, na hata safari za kawaida,” alisema Mvamba kwa niaba ya viongozi hao.
Kwa mujibu wa viongozi hao, maendeleo ya uwanja wa ndege huo pia yanachangia pato la Iringa Vijijini, mkoa wa Iringa na taifa kupitia kodi na ushuru mbalimbali.
Sambamba na hilo, viongozi hao wametoa wito kwa serikali kuendelea kuwekeza zaidi katika miundombinu ya anga ili kuongeza manufaa kwa wananchi na kukuza uchumi.
Uwanja wa Ndege wa Iringa ni kiungo muhimu cha maendeleo endelevu, ukiimarisha mtiririko wa watu, bidhaa, na huduma kwa kasi inayochochea ukuaji wa uchumi, kwa kuwa na safari za moja kwa moja kati ya Iringa na Dar es Salaam, uwanja huu unarahisisha biashara, unafungua milango kwa uwekezaji wa kimkakati, na kuimarisha sekta ya utalii kwa kuwavutia wageni wa ndani na nje ya nchi na pia kutoa msukumo kwa mnyororo wa thamani wa kilimo na viwanda, kwa kuwawezesha wazalishaji wa ndani kufikia masoko ya kitaifa na kimataifa kwa ufanisi zaidi.
Kwa mantiki hiyo, uwekezaji endelevu katika miundombinu ya anga si tu kwamba unakuza ustawi wa jamii, bali pia unahamasisha ukuaji wa uchumi shirikishi unaowanufaisha wananchi wote.