▪️Hatua hiyo kuongeza uzalishaji wa madini nchini
▪️Nyamongo kuanzishwa Kituo cha Elimu ya Uchenjuaji Madini
▪️Wachimbaji Wadogo wampongeza Rais Samia juu mafanikio sekta ya Madini
▪️Waziri Mavunde asisitiza juu ya uwezeshwaji Watanzania kimtaji
*Musoma,Mara*
Serikali kwa ushirikiano na sekta binafsi imejipanga kuanzisha vituo vya ukodishaji mitambo ya uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kutumia teknolojia za kisasa kufanya shughuli zao kwa tija.
Hayo yamesemwa leo tarehe 06 Juni, 2025 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde wakati akihitimisha Kongamano la Maonesho ya Madini mkoani Mara kwenye viwanja vya Mukendo vilivyopo Manispaa ya Musoma.
“Sote tunatambua kwamba wachimbaji wadogo hawana uwezo wa kununua na kuihudumia mitambo ya kisasa kama kwa ajili ya uchimbaji,” amesema Mavunde.
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameilekeza Wizara ya Madini kuja na mpango huo ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata fursa ya kutumia teknolojia ya kisasa kwenye shughuli zao lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa madini,” amesema Waziri Mavunde.
Sambamba na Mitambo ya kukodisha amesema Serikali inatarajia pia kuanzisha Kituo cha Elimu ya Uchenjuaji wa madini ambacho kitakuwa na Mtambo wa Uchenjuaji wa madini eneo la Nyamongo-Tarime.
Ameongeza kwamba ni matarajio kwamba mpango huo unakwenda kubadilisha uchumi wa wachimbaji wadogo kwa kuinua vipato vyao na hatimaye kuongeza mchango zaidi kwenye ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na sekta ya Madini.
Awali, akisoma taarifa ya sekta ya madini kwa Mkoa wa Mara, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara Mhandisi Amin Msuya amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Mhe. Rais, Mkoa wa Mara umezalisha dhahabu tani 58.90 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 6.90 kwa wachimbaji wadogo, kati na wakubwa.
Akitoa salamu za wachimbaji, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania ( FEMATA) Bw. John Bina amempongeza Mhe Rais Samia Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye sekta ya madini na kutoa rai kwa wachimbaji wadogo kuchangamkia fursa zilizopo Mkoani Mara na kuwahimiza kufuata Sheria na taratibu zilizowekwa kwani Serikali imeziboresha ili kulinda maslahi ya wachimbaji wadogo nchini.
Naye , Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Mtambi amereleza kwamba lengo la kongamano hilo ni kuleta pamoja wadau wa sekta kujadili fursa zilizopo mkoani Mara na namna ya kuzifikia. Aidha, ameaisitiza kuwa kongamano hilo litaendelea kufanyika kila mwaka ili liwe chachu ya kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye GDP ya Mkoa ambao kwa sasa umefikia asilimia 18.