Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini, kwa lengo la kuboresha ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo ya Amali na kuongeza ubora wa elimu.
Mageuzi hayo pia yana lengo la kuhamasisha fikra tunduizi (Critical Thinking) miongoni mwa wanafunzi ili waweze kuwa wabunifu na wavumbuzi wa masuala mbalimbali kwa kutumia sayansi na teknolojia.
Hayo yamesemwa Machi 28, 2025 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda, wakati akifunga mafunzo ya walimu wa shule za Sekondari wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati yaliyofanyika mkoani Singida.
Prof. Mkenda amesema kuwa Serikali imejipanga kuimarisha ubora wa elimu nchini kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP), ambao unawapa walimu mbinu bora na za kisasa ili kuwafundisha wanafunzi.
Amesema mradi huo unalenga kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha masomo ya Sayansi na Hisabati kwa njia bora, ili wanafunzi waweze kuelewa na kumudu masomo hayo kwa ustadi na ufanisi mkubwa, na kwamba mafunzo hayo yatakuwa endelevu.
“Kupitia mafunzo haya, tunatarajia kuona ongezeko la wanafunzi wenye uwezo mkubwa wa kuelewa masomo wanayofundishwa na kuwa na ujuzi utakaowasaidia kuwa na fikra tunduizi. ufanisi huo utatokana na walimu kuwawezesha wanafunzi kuchambua, kutafakari, na kutatua changamoto kwa kutumia maarifa waliyonayo,” amesema Mkenda na kuongeza.
“Haya ni baadhi ya matunda ya utekelezaji wa maagizo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alisisitiza katika uzinduzi wa sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) kuwa mageuzi ya elimu yawe ya kitaalam na yazingatie maoni ya wataalam ili kuboresha sekta ya elimu, yakiangazia si tu utoaji wa elimu bora, bali pia uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa walimu, ili waweze kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa,” Mkenda .
Akizungumzia maendeleo ya Sekta ya Elimu, Waziri Mkenda amesema kupitia Dkt.Samia Scholarship, zaidi ya wanafunzi 600 waliomaliza kidato cha sita na kufaulu kwa alama za juu katika masomo ya sayansi na hisabati wamepata ufadhili wa kusoma vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuwavutia wanafunzi kupenda na kusoma masomo ya sayansi na hisabati ili kuwa na idadi kubwa ya wataalam watakaolisaidia Taifa.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Mafunzo ya Ualimu nchini, Huruma Mwageni, amesema kuwa mradi wa SEQUIP umefanikisha walimu 40,000 wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati katika mikoa yote ya nchi.
“Malengo ya mradi yamefikiwa kwani dhamira yetu ilikuwa ni kuwafikia walimu wote 40,000 wanaofundisha masomo hayo, na wamejifunza mbinu mpya na bora za kufundisha zinazozingatia mazingira yanayowazunguka na matumizi ya Tehama ili kuwavutia wanafunzi,” Mwageni .
Muwakilishi kutoka TAMISEMI, Singo Yusuph, amesema ana imani kuwa wanafunzi wengi watavutiwa kusoma masomo ya sayansi kwa sababu walimu wamejengewa uwezo wa kufundisha mada ngumu kwa njia rahisi. Aliongeza kuwa watafuatilia matokeo ya mafunzo hayo maeneo yote nchini ili kuona ufanisi wake.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, amesema kuwa wao ni wanufaika wa miradi mingi ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule ya kisasa ya mafunzo ya amali, ambayo itajengwa kwa gharama ya bilioni 1.5.
Ameongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejitahidi kuboresha mazingira ya walimu, yakiwamo maslahi yao.