Na Helena Magabe, Tarime
Mwalimu wa watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Magufuli, Mekaus Maingu, ameomba serikali kuongeza walimu wa nukta nundu pamoja na mashine za nukta nundu kutokana na upungufu uliopo shuleni hapo. Maingu amesema kuwa shule hiyo ina mashine moja tu ya nukta nundu, hali inayomlazimu kufundisha vipindi 86 kwa wiki, kuanzia chekechea hadi darasa la sita.
Maingu ametoa ombi hilo Machi 27, 2025, wakati Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo. Miradi aliyokagua ni pamoja na ujenzi wa choo chenye matundu manne, umaliziaji wa bweni la wasichana na uzio wa bweni hilo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Magufuli, Muguta Manunguli, amesema kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 131, wakiwemo wenye ulemavu wa akili 105, wenye ulemavu wa kusikia 19 na wenye ulemavu wa kuona saba. Manunguli amesema kuwa shule hiyo ina walimu 11 pekee huku ikiwa na upungufu wa walimu 10. Ameiomba serikali kuongeza walimu na wataalamu wa elimu ya viungo ili kusaidia maendeleo ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Turwa, Fredrick John, amesema kuwa mnamo Aprili 20, 2023, shule hiyo ilipokea shilingi milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa bweni la wasichana. John amesema kuwa lengo la ujenzi huo ni kuimarisha usalama wa wanafunzi, kupunguza upotevu wa mali zao na kuzuia mwingiliano wa watu wasiohusika katika mazingira ya bweni. Amesema kuwa shilingi milioni 25.5 zilitumika kununua vifaa vya ujenzi na shilingi milioni 4.5 zilitumika kwa malipo ya mafundi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa shule hiyo, Naftali Philipo Akyoo, amesema kuwa uwepo wa kituo hicho umechangia kuondoa watoto wenye mahitaji maalumu waliokuwa wakifichwa majumbani. Akyoo amesema kuwa iwapo kituo hicho kitapata miundombinu bora, idadi ya watoto wanaojiunga na shule hiyo itaongezeka zaidi.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Msati Highway, Halima Bwile, ameishukuru serikali kwa juhudi zake za kuboresha elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu. Bwile amewasihi wazazi kutowaficha watoto wao majumbani na badala yake wawapeleke shuleni ili wapate haki yao ya elimu.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha wanasimamia kwa umakini matumizi ya fedha za serikali ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa. Gowele amesema kuwa serikali inatambua changamoto zinazoikabili shule hiyo na kwamba mwitikio wa wananchi kwa shule hiyo maalumu umekuwa mkubwa, kwani idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka sita hadi 131.