Serikali imeipongeza Shule ya Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam kutokana na mafanikio ya kitaaluma na mchango wake kwa serikali katika sekta ya elimu.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na Mdhibiti Ubora wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Albert Mutalemwa wakati wa mahafali ya shule ya awali na msingi Hazina jijini Dar es Salaam.
Kwenye matokeo ya shule hiyo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), wanafunzi wote 27 wa shule hiyo walipata alama A kwenye masomo yote. Amesema kiwango kikubwa cha maarifa walichoonesha wanafunzi wa shule hiyo kwenye maonesho mbalimbali ya kitaaluma kinadhihirisha elimu bora inayotolewa na shule hiyo.
Amesema wanafunzi hao wameonesha umahiri wa hai ya juu kuelezea masuala mbalimbali yakiwemo ya sayansi na tiba ya magonjwa mbalimbali kana kwamba ni madaktari.
“Walimu kwa upande wao wanafundisha vizuri sana na mmeona namna gani watoto wameelezea kwa umahiri wa hali ya juu hapa lakini wazazi mnapokuwa nyumbani hakikisheni watoto wanakuwa na maadili mema na waepuka kukaa na makundi yanayoweza kuwasababishia kupata tabia za ovyo,” amesema na kuongeza,
“Nimeambiwa hapa kwamba kuna wageni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) sasa kuwepo kwa wageni hawa kunaonesha kwamba shule hii iko vizuri sana kwenye uhusiano wa kimataifa ambayo inaweza kuwasaidia wanafunzi wa shule hii kupata fursa za kimataifa”.
Wanafunzi wa shule hiyo wameonesha umahiri wa hali ya juu kwenye maonesho mbalimbali ya kitaaluma kiasi cha kuwashangaza wazazi na wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo.
Miongozi mwa maonesho waliyofanya ni kuonesha namna ya kutibu ugonjwa wa ini na kutoa maelezo ya kina ya namna mtu anavyoweza kulinda afya yake kwa kubadili mtindo wa maisha na kula kwa kuzingatia afya.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Omari amewashukuru wazazi kwa kuwaamini na kuwapa watoto wao wawafundishe na ameahidi kuwa wataendelea kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri kwenye mtihani ya kitaifa.
“Tumekuwa tukifanya vizuri sana na kushika nafasi ya kwanza kwenye mitihani kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na kitaifa kama mlivyoona matokeo ya mwaka huu lakini ninawahakikishia wazazi hatutabweteka, na badala yake tutahakikisha tunabaki kwenye ubora ule ule,” amesema.
Amesema wanafunzi wa shule hiyo hivi karibuni walialikwa kutoa mada kuhusu mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa (UN), ambapo Waziri wa Ulinzi aliyekuwa mgeni rasmi amewapongeza kwa kujiamini na kutoa mada ambayo iliwasisimua wageni waalikwa.
“Wanafunzi wa Hazina wamefundishwa kujiamini na kuzungumza kwa lugha ya Kiingereza kwa ufasaha mbele za watu, na ndiyo sababu walichaguliwa kwenda kwenye siku ya Umoja wa Mataifa, walizungumza na walikonga nyoyo za wageni waalikwa,” amesema