Wakati hofu ikitanda miongoni mwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na Ludewa kuhusu kusimama kwa ujenzi wa barabara kuu ya Itoni-Lusitu kwa takriban mwaka mmoja, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika, amewatoa hofu kwa kueleza kuwa kazi hiyo itaendelea mara baada ya msimu wa mvua kumalizika.
Akizungumza wakati wa kusoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kipindi cha miaka minne (2020-2024), Mwanyika alifafanua kuwa kusimama kwa ujenzi wa barabara hiyo haukutokana na uzembe au kutelekezwa, bali ulisababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana na kuathiri maeneo mengine nchini, jambo lililosababisha rasilimali fedha na vifaa kuhamishwa kwa dharura.

“Barabara hii ilikuwa ijengwa kwa miaka miwili na ujenzi wake ulianza haraka sana lakini kwa bahati mbaya kwa kipindi cha mwaka mmoja mkandarasi hayupo site na nitoe sababu kwa kuwa kuna watu wanawaza barabara hii imetelekezwa niwaambie barabara hii haijatelekezwa, sote ni mashahidi mwaka jana kulikuwa na mvua zisizo za kawaida lakini Njombe mjini hatukuona sana hizo mvua na madhara yake lakini wenzetu Kibiti, Lindi, Mafya maji yalikuwa kwenye mapaa ya nyumba”, amesema Mbowe.
Mwanyika amesema mara baada ya hali hiyo serikali ilifanya maamuzi ya kusaidia wananchi kwenye maeneo yaliyokuwa yamepata tatizo kubwa kwa kupunguza kasi ikiwemo kuondoa baadhi ya vifaa na rasilimali fedha kwenda kutatua changamoto kwenye maeneo yenye shida kubwa.

“Kwa hiyo ndugu zangu barabara hiyo ilisimama kwasababu hizo sio kwa kutelekezwa ila ni kwasababu ilionekana rasilimali ziende kusaidia maeneo ambayo yamekuwa ni hatari na tunashukuru Waziri wa Ujenzi ametuhakikishia kuwa kipindi hiki fedha zitaletwa kwa hiyo tunauhakika mvua zikiisha mkandarasi ataendelea na kazi”, amesema Mwanyika