Latest Posts

SERIKALI YAZINDUA SHAMBA DARASA LA KILIMO BIASHARA

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imezindua rasmi Mwongozo wa kuanzisha na kuendesha Shamba Darasa la Kilimo Biashara, ikiwa ni hatua madhubuti ya kuhakikisha huduma za ugani na mafunzo kwa wakulima zinatolewa kwa ufanisi na kwa kufuata mfumo mmoja wa kitaifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema  kuwa kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakipokea taarifa na maelekezo tofautitofauti kutoka kwa taasisi mbalimbali, hali iliyowachanganya na kuathiri ufanisi wa shughuli zao za kilimo.

“Wakulima wetu hawana shida ya kujua fedha zinatoka wapi, shida yao kubwa ni kupata huduma sahihi na zenye ufanisi, hatuwezi kuwa na miongozo mingi ambapo kila asasi inakuja na mwongozo wake tofauti, leo mkulima yupo kwenye semina ya CARE, kesho ya World Vision, kila mmoja anakuja na vipimo vyake – mmoja anasema panda kwa sentimita sita, mwingine anasema sentimita ishirini, hali hii haiwezi kuendelea,” amefafanua  Bw. Mweli.

Amesema  kuwa ili kuongeza thamani ya fedha zinazotolewa na wadau kwa ajili ya maendeleo ya kilimo, sasa kutakuwa na mwongozo mmoja wa kitaifa ambao wote – serikali, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo – watapaswa kuufuata na kuutekeleza kwa pamoja.

Bw. Mweli ameeleza kuwa mwongozo huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya CARE International na Wizara ya Kilimo, na kwamba licha ya kufadhiliwa na shirika hilo, umeidhinishwa rasmi na serikali, hivyo kuwa mwongozo wa serikali unaotekelezwa kitaifa.

“Tulisisitiza hatutashiriki hadi tujiridhishe kuwa mwongozo huu unalenga kweli kumwinua mkulima wa kawaida, tumeusoma, tumeuridhia na sasa tupo tayari kuutekeleza kwa pamoja.

“Nanyi mtakubaliana nami kuwa baadhi ya mambo yaliyokuwa yamepitwa na wakati sasa yamefanyiwa kazi, lengo letu ni kuhakikisha shughuli zote za kilimo zinafanyika kwa muundo unaofanana na ulio thabiti,” amesema.

Mwongozo huu unatarajiwa kuwa chombo muhimu katika kuboresha mafunzo ya vitendo kwa wakulima kupitia mashamba darasa, kuongeza tija na kuongeza kipato cha wakulima wa Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!