WANANCHI wa Kijiji Cha Kwasadala Kata ya Masama Kusini Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro wakiongozwa na Diwani wa Kata hiyo Cedrick Pangani wameshiriki zoezi la upandaji miti rafiki wa mazingira zaidi ya 1,000 katika shule Mpya ya Msingi Kwasadala iliyokamilika kwa zaidi ya asilimia tisini,ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Zoezi hilo limefanyika Aprili 7,2025 sambamba na jitihada za jamii kuunga mkono maendeleo ya elimu, ambapo shule hiyo mpya imejengwa kwa lengo la kuwa mkombozi kwa wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata elimu katika shule za mbali.
Pangani amesema kuwa upandaji huo wa miti ni hatua ya kimkakati ya kuhakikisha shule hiyo mpya inakuwa na mazingira rafiki, ya kijani na salama kwa wanafunzi na walimu ikiwa ni pamoja na kuacha alama kama Kiongozi kwa miaka mitano baada ya kutoa ahadi hiyo.
“Tunataka watoto wetu wasome kwenye mazingira bora. Hii miti tuliyopanda leo itasaidia kupunguza joto, kuimarisha afya ya hewa na pia kuwa kivuli kwa watoto wetu,” amesema Diwani huyo.
Kwa upande wao Wananchi akiwemo Godwin Killeo ameeleza kuwa wanathamini mchango wa shule hiyo katika kupunguza changamoto za elimu, hasa kwa watoto waliokuwa wakilazimika kuamka alfajiri kwenda umbali mrefu kutafuta elimu huku wakikumbana na changamoto za ajali wakati wakuvuka barabara na wengine kukatisha masomo yao kwa kuchoka umbali mrefu
Afisa Maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Hai John Katikiro amesema kuwa wamepada miti zaidi ya elfu Moja katika Shule hiyo huku wazazi walioshiriki zoezi hilo wakipatiwa miti ya kupanda katika malazi yao.
“Tuna lengo la kupanda miti Milioni Moja kwa mwaka katika wilaya yetu na zoezi hili ni muendelezo kitakachofuata hapa ni upandaji wa miti ya matunda ili Wanafunzi wapate matunda shuleni” John
Zoezi hilo limeacha alama ya matumaini kwa wakazi wa Masama Kusini na linatarajiwa kuwa chachu ya shughuli nyingine za maendeleo katika sekta ya elimu na mazingira.