Latest Posts

SHURA YA MAIMAMU YATOA WITO KWA RAIS SAMIA KUHUSU MAREKEBISHO YA UCHAGUZI

Shura ya Maimamu Tanzania imetoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuitisha kikao cha wadau wa siasa ili kufanya marekebisho ya mifumo ya uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Shura hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda, wakati wa Baraza la Eid lililofanyika katika Msikiti wa Tungi, Dar es Salaam.

Malalamiko ya Vyama vya Upinzani

Sheikh Ponda amesema wito huo umetokana na malalamiko ya vyama vya Chadema Tanzania Bara na ACT Wazalendo Zanzibar, ambavyo vimeendelea kulalamikia mfumo wa uchaguzi.

“Kauli ya CHADEMA ‘No Reform, No Election’ na ya ACT Wazalendo ya kupinga uchaguzi wa siku mbili Zanzibar zinaakisi malalamiko ya uchaguzi mbovu kama ule wa Serikali za Mitaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020, na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024,” alisema Sheikh Ponda.

Ameeleza kuwa hata baadhi ya viongozi wa serikali, wanasheria na viongozi wa dini wamekiri kuwa chaguzi zilizopita zilikuwa na kasoro kubwa mno.

Hatari kwa Usalama wa Taifa

Sheikh Ponda ameonya kuwa kuendelea kwa kasoro hizi kunaweza kuhatarisha usalama wa nchi.

“Mfumo wa sasa unapoka haki za wananchi za kidemokrasia na kuhatarisha usalama wa taifa. Tunatoa wito kwa Rais Samia kuitisha kikao cha wadau wa siasa kujadili mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025,” alisisitiza Sheikh Ponda.

Maswali Juu ya Ushiriki wa Jeshi Katika Uchaguzi

Shura ya Maimamu pia imeshtushwa na kauli ya Rais Samia ya kulitaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiandaa kwa uchaguzi.

“Suala la uchaguzi ni la kiraia, si la kijeshi. Jeshi halipaswi kuhusika na uchaguzi,” alisema Sheikh Ponda, akiongeza kuwa Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa ndizo taasisi zinazopaswa kusimamia uchaguzi wa kiraia.

Wito wa Kufutwa kwa Sheria Kandamizi

Shura hiyo pia imetoa wito kwa Bunge la Tanzania kufuta sheria zote kandamizi, ikiwemo Sheria ya Ugaidi.

“Sheria hii imekuwa ikitumika dhidi ya Waislamu na inawanyima haki zao za msingi. Ni muhimu ifutwe,” alisema Sheikh Ponda.

Pia ameitaka serikali kuwasilisha ushahidi mahakamani kwa watuhumiwa wa mashauri ya ugaidi ili kupata haki zao.

“Ni kinyume na haki za binadamu kuwaweka watu gerezani kwa miaka 10 bila hatia kuthibitishwa na mahakama,” alihitimisha Sheikh Ponda.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!