Katibu Mkuu wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO) anayemaliza muda wake, Jens Stoltenberg, ameweka wazi kuwa mustakabali wa amani nchini Ukraine utategemea sana msaada wa kijeshi unaoendelea kutolewa kwa taifa hilo, huku akisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya amani na Urusi.
Akizungumza katika hotuba yake ya kuaga kabla ya kuondoka kwenye wadhifa wake, Stoltenberg amesema kuwa mazungumzo ya amani kati ya Ukraine na Urusi yatakuwa magumu, lakini ni muhimu na yatafanikiwa tu kwa msaada wa ulinzi thabiti.
“Nguvu za kijeshi ni sharti la mazungumzo,” alisema Stoltenberg. “Lazima tuzungumze na majirani zetu, bila kujali ugumu wa mazungumzo hayo, lakini mafanikio yatapatikana ikiwa mazungumzo hayo yatalindwa na ulinzi imara.”
Stoltenberg alibainisha kuwa usambazaji wa silaha kwa Ukraine siyo tu unaimarisha ulinzi wa nchi hiyo, bali pia unaongeza uwezekano wa kufikia amani ya kudumu kwa kuzuia jitihada za Urusi kutumia nguvu.
Katika kuzungumzia athari za kijeshi, Stoltenberg pia alikiri kuwa nguvu za kijeshi zina mipaka yake, akitoa mfano wa Afghanistan. Hata hivyo, aliendelea kueleza kuwa njia pekee ya kumshinikiza Rais Putin kutambua haki ya kidemokrasia ya Ukraine ni kuendelea kutoa msaada wa kijeshi.
“Tunapaswa kumfanya Putin atambue kuwa hawezi kupata anachotaka kwa nguvu, na kwa kuifanya iwe ya gharama kubwa kiasi kwamba atalazimika kukiri haki ya Ukraine kubaki nchi huru ya kidemokrasia,” alisema.
Stoltenberg alisisitiza zaidi kuwa mafanikio yoyote ya baadaye lazima yahusishe dhamana thabiti ya usalama kwa Ukraine, ambayo inamaanisha uungaji mkono wa kijeshi wa muda mrefu na uanachama wa NATO.
“Mlango wa NATO uko wazi, na Ukraine itajiunga,” alithibitisha Stoltenberg, akiongeza kuwa usalama wa Ulaya hauwezi kuimarishwa bila Ukraine kuwa mwanachama wa muungano huo.