Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omary Sukari, amesema kuwa tasnia ya ualimu ni muhimili muhimu katika maendeleo ya nchi kutokana na mchango mkubwa wa walimu katika kuwaandaa wanafunzi kuwa raia bora wa baadae.
Dkt. Sukari aliyasema hayo alipomwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita kwenye uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Geita. Alieleza kuwa serikali inatambua na kuthamini jitihada kubwa zinazofanywa na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanalelewa na kufundishwa kwa weledi ili waweze kuwa na mchango chanya kwa jamii.
“Walimu wanafanya kazi kubwa sana ya kuwajenga wanafunzi kimaadili na kielimu. Bila wao, hatuwezi kupata wataalamu bora wa baadae,” alisema Dkt. Sukari.
Aidha, alibainisha kuwa serikali imeendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule mpya pamoja na nyumba za walimu, hatua ambayo imeongeza ari na motisha kwa walimu kufanya kazi kwa bidii.
Kwa upande wake, Katibu wa CWT Mkoa wa Geita, Pauline Tinda, ameishukuru serikali kwa jitihada zake katika kuboresha miundombinu ya elimu. Amesema maboresho hayo yamechangia kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu wakati wa ufundishaji.
“Tunaishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia. Hii imerahisisha kazi yetu na kuongeza ufanisi,” alisema Tinda.