Latest Posts

TAIFA TEK NA LYRA IN AFRICA ZASAINI MAKUBALIANO; SHULE ZA SERIKALI IRINGA KUPATA KOMPYUTA NA UJUZI WA AI.

Serikali imeendelea kupiga hatua katika kuimarisha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu unaosisitiza mafunzo ya amali na ujuzi wa vitendo, baada ya zaidi ya wanafunzi mia tatu pamoja na walimu mia moja kutoka shule kumi za serikali mkoani Iringa kutarajiwa kunufaika na mafunzo ya TEHAMA kwa kipindi cha miaka miwili.

Kupitia mpango huo wa kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi, shule hizo zitapatiwa kompyuta pamoja na mafunzo maalum ya TEHAMA, yakiwemo matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence) hatua  inayolenga kuongeza ujuzi wa vitendo, kukuza ubunifu na kuboresha ufundishaji pamoja na ujifunzaji darasani.

Akizungumza wakati wa kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Kituo cha Teknolojia na Ubunifu cha Taifa Tek na Shirika la Lyra in Africa, Mkurugenzi wa Taifa Tek, Said Hoza, amesema mradi huo unalenga kuwafanya wanafunzi wa shule za serikali kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Lyra in Africa, Dkt. Gerald Gindo, amesema uwekezaji katika TEHAMA mashuleni ni msingi muhimu wa kuandaa kizazi chenye uwezo wa kujiajiri na kushindana katika soko la ajira la sasa na la baadaye.

Naye Mratibu wa Mpango wa Kusambaza Ujuzi Shuleni, Konzo Ikweta, amesema mbali na kugawa vifaa, pia kutakuwa na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha walimu na wanafunzi wananufaika ipasavyo na mafunzo hayo.

Mpango huo unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya elimu mkoani Iringa, ukiunga mkono jitihada za serikali za kujenga mfumo wa elimu unaozalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kujitegemea.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!