Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka John Mwambage, ametoa ufafanuzi kuhusu tukio lililotokea Machi 13, 2025, katika kituo cha mizani cha Vigwaza, ambapo gari lililokuwa likisafirisha mzigo wa shaba (copper) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lilipata changamoto ya uzito.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, Mhandisi Mwambage alieleza kuwa shughuli za upimaji wa uzito barabarani zinafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2018. Alisisitiza kuwa mizani ya Vigwaza hufanyiwa ukaguzi kila baada ya miezi mitatu na Wakala wa Vipimo (WMA) ili kuhakikisha ufanisi wake. Mara ya mwisho uhakiki ulifanyika Februari 15, 2025.
Mhandisi Mwambage aliendelea kwa kusema kuwa TANROADS inawasisitiza wasafirishaji kufuata sheria na kufikisha malalamiko yao kwa mujibu wa utaratibu.
“Ikitokea changamoto kwenye mizani yoyote nchini, wasafirishaji wanapaswa kueleza malalamiko yao kwa Mkuu wa Mizani, Meneja wa TANROADS wa Mkoa husika, au iwapo suala lina sura ya rushwa, wawasiliane na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Kama majibu hayawaridhishi, wanaweza kufikisha suala hilo kwa Mtendaji Mkuu wa TANROADS au Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,” alisema Mhandisi Mwambage.
Kwa mujibu wa Vicent Tamo, mwakilishi kutoka TANROADS Makao Makuu anayesimamia shughuli za mizani, gari lenye namba za usajili T137 DLQ (kichwa) na T567 CUR (tela), lilipimwa kwenye mizani ya Vigwaza Kaskazini na kubainika kuwa na uzito uliozidi kiwango kilichowekwa kisheria.
Kwa mujibu wa sheria, gari hilo lilipaswa kubeba tani 48,000 lakini lilipimwa na kubainika kuwa na tani 48,150, ikiwa na ongezeko la kilo 150. Aidha, ilibainika kuwa kwenye differential axle (mtaimbo wa katikati, maarufu kama “diff”), gari lilizidisha uzito kwa kilo 1,450 nje ya kiwango kinachoruhusiwa.
Dereva wa gari hilo alipinga matokeo ya upimaji huo na kudai kuwa alishapita kwenye mizani nyingine bila tatizo, akihisi kwamba uzito wake umeongezwa isivyo halali.
Tamo amefafanua kwa kusema kuwa, mizani hiyo ni ya kidijitali (automated) na haipimwi kwa makadirio ya binadamu. Uzito unachukuliwa moja kwa moja na mfumo wa kielektroniki, hivyo hakuna uwezekano wa kufanyiwa udanganyifu.
“Mzani huu hauandiki uzito kwa makadirio ya binadamu. Ni mfumo wa kielektroniki unaorekodi uzito halisi wa gari pindi linapopita,” alisema Vicent Tamo.
Sheria ya Udhibiti wa Uzito wa Magari Afrika Mashariki inamtaka msafirishaji aliyezidisha uzito kulipa tozo ya uzidishaji, kisha ashushe au apange upya mzigo wake kabla ya kurudi kupima. Ombi la kupima gari mara ya pili halikukubalika kwa sababu ni kinyume cha utaratibu wa kisheria.
Katika ufuatiliaji wake, TANROADS iligundua kwamba gari hilo lilikuwa limepimwa katika mizani mbalimbali kabla ya kufika Vigwaza. Mizani ya Kafulafuta (Zambia), Mpika (Zambia), na Makambako (Tanzania) zote zilionesha uzito uliozidi kiwango cha kisheria, na tofauti kubwa ya uzito kati ya mizani hizi inaonyesha uwezekano wa hitilafu kwenye mfumo wa air suspension (booster) wa gari, ambapo uzito hubadilika kulingana na mgandamizo wa hewa kwenye ekseli.
Aidha, imeelezwa kuwa changamoto hiyo ilitokana na ukosefu wa uelewa wa kutosha kuhusu mifumo ya gari, hususan mfumo wa air suspension, jambo lililosababisha sintofahamu kwa dereva.
TANROADS ilifanya jitihada za kumuelimisha mmiliki wa gari husika kuhusu sheria na taratibu za udhibiti wa uzito barabarani. Baada ya maelezo kutolewa, mmiliki alielewa na kuridhia kufuata utaratibu wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kukamilisha taratibu za malipo ya tozo husika ili kuruhusu gari kuendelea na safari.
Baada ya kukamilika kwa taratibu zote, gari hilo liliendelea na safari yake bila kikwazo chochote. TANROADS inaendelea kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya usafirishaji ili kuhakikisha sheria za udhibiti wa uzito wa magari zinafuatwa kwa manufaa ya wote.