Sekta ya kifedha nchini Tanzania imehimiza matumizi ya teknolojia na kidijiti kama njia kuu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha kuwa matumizi ya sayansi, teknolojia, na kidijiti yanapewa uzito mkubwa katika Rasimu ya Dira 2050.
Akizungumza katika Mkutano wa Taasisi za Kifedha Kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Serena mkoani Dar es Salaam, Jumatano tarehe 18 Desemba 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Bi. Tuse Joune, ameeleza jinsi teknolojia inavyoweza kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa taifa.
“Tanzania imeweka msingi madhubuti na mifano halisi katika sekta ya kifedha, mawasiliano ya simu, afya, na usafirishaji. Tunapaswa kuwekeza vya kutosha na kwa kimkakati katika eneo hili ili kupata manufaa halisi,” amesema.
Ametoa mfano wa jinsi sekta ya benki imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha huduma za kidijiti kwa kushirikiana na sekta ya mawasiliano, akibainisha kuwa uchumi wenye nguvu unahitaji sekta ya kifedha inayotumia teknolojia kusaidia ukuaji wa sekta nyingine.
“Maendeleo ya kiteknolojia katika utoaji wa huduma za kibenki yanaonesha kuwa sekta ya kifedha tayari ina msingi thabiti wa matumizi ya teknolojia na sayansi. Teknolojia inatoa suluhisho la changamoto za uzalishaji, kuongeza thamani, na usambazaji wa bidhaa, huku ikiimarisha uwezo wa ukuaji wa sekta za kiuchumi na kijamii nchini Tanzania,” amesema.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika sekta ya kifedha si muhimu tu kwa kuboresha huduma za kifedha bali pia kwa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya kifedha na sekta nyingine zenye kipaumbele katika Dira ya 2050.
Kwa upande mwingine Bi. Joune ametaja maeneo kadhaa yanayohitaji kuimarishwa katika Rasimu ya Dira ya Maendeleo 2050, ikiwamo eneo la ufadhili wa ubunifu.
“Tunapendekeza kuwa sehemu hii iongeze umuhimu wa taasisi za kifedha za maendeleo kama vile TIB, TADB, na TMRC. Taasisi hizi zinapaswa kupata msaada wa serikali ili ziweze kutoa ufadhili wa muda mrefu kwa miradi mikubwa,” amesema.
Bi. Joune amebainisha kuwa ukosefu wa ufadhili wa muda mrefu umekuwa changamoto kubwa katika sekta ya kifedha ya Tanzania.
“Kwa miaka mingi, tumekuwa tukijadili changamoto ya riba kubwa katika mikopo, lakini tatizo kubwa ni kutokuwepo kwa ufadhili wa muda mrefu. Miradi mingi inahitaji ufadhili wa muda mrefu, lakini benki zinaweza kutoa mikopo ya muda mfupi pekee,” ameeleza.
Halikadhalika Bi. Joune amesisitiza umuhimu wa masuala ya Mazingira, Jamii, na Utawala (ESG) kama sehemu muhimu ya Dira 2050. Amesema kuwa masuala haya ni muhimu sio tu kwa sekta ya kifedha bali pia kwa maendeleo endelevu ya taifa.
“Ni jambo la kutia moyo kujifunza umuhimu wa masuala ya ESG na masuala ya mabadiliko ya tabianchi ndani ya Dira ya 2050. Hili si muhimu tu kwa sekta ya benki na kifedha kwa ujumla, bali pia kwa uendelevu wa siku zijazo wa matokeo ya maendeleo yanayotarajiwa kufanikishwa na dira hii.” amesema.
Aisha Bi. Joune ameiihimiza serikali na wadau wengine kuwekeza katika kuimarisha taasisi za kifedha za maendeleo na kuhakikisha kuwa dira ya taifa inakuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha uchumi wa nchi.
“Sekta ya kifedha ina jukumu kubwa katika kufanikisha dira ya maendeleo ya taifa. Ni jukumu letu kuhakikisha tunatoa mchango wetu kikamilifu,” amehitimisha.