Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) leo tarehe 24 Oktoba 2024 imekutana na Mhandisi wa miradi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF)Tanzania , Mhandisi Mohamed Hindi, kujadili utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu katika shule 13 za msingi na sekondari katika mikoa ya Kigoma, Tabora, na Songwe.
Mradi huu unatekelezwa kwa ufadhili wa UNICEF Tanzania kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, na utakapokamilika unatarajia kuwanufaisha wanafunzi takriban 3,800 kupata mazingira bora ya kujifunzia.
Katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya TEA, Ilazo, Jijini Dodoma, pande zote mbili zimepitia utekelezaji wa mradi huo ulioanza mwezi MeiJulai 2024 na unatarajia kukamilika mwezi Oktoba 2024 ukidumu kwa miezi mitatu.
Tathmini hiyo imebainisha mafanikio na changamoto zilizojitokeza, huku ikijadiliwa mbinu bora za kutatua changamoto hizo.
Akizungumza katika tathmini hiyo, Mhandisi Hindi alisema kuwa mradi huo umelenga kukabiliana na upungufu wa maabara za sayansi katika shule za sekondari, pamoja na kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi.
Kiasi cha Shilingi milioni 824 zimetumika katika awamu ya kwanza ya mradi huo, kati ya Shilingi Bilioni 2.5 zilizopangwa kutumika katika awamu mbili.
Mhandisi Hindi alieleza kuwa utekelezaji wa mradi kwa ujumla ni wa kuridhisha, lakini alitaja maeneo machache yanayohitaji kuboreshwa ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi zaidi.
Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Raslimali na Usimamizi wa Miradi wa TEA, Bw. Masozi Nyirenda, aliihakikishia UNICEF Tanzania kuwa miradi hiyo itatekelezwa kwa viwango vinavyotarajiwa, na timu ya wataalamu wa TEA iko tayari kufanyia kazi mapendekezo ya maboresho yaliyotolewa na UNICEF Tanzania.
Mfuko wa Elimu wa Taifa, unaosimamiwa na TEA, una jukumu la msingi la kutafuta rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya kusaidia jitihada za Serikali za kuwezesha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa nchini.