Latest Posts

TEA, UNICEF TANZANIA WAJADILI UTEKELEZAJI MIRADI YA ELIMU

Katika kuimarisha maendeleo ya sekta ya elimu nchini, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imekutana na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) leo Mei 14, 2025, katika ofisi za TEA zilizopo Ilazo Dodoma. Lengo la kikao hicho ni kujadili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu inayofadhiliwa na UNICEF kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kufanikisha utekelezaji wa sera na mikakati ya serikali katika sekta ya elimu.

Kikao hicho kiliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha, ambapo miradi mikuu iliyojadiliwa ni pamoja na miradi 34 ya miundombinu ya elimu katika mikoa ya Kigoma, Songwe na Tabora, utekelezaji wa miradi 7 ya Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu (IPOSA), pamoja na ujenzi wa maabara 52 katika mikoa ya Simiyu na Dodoma. Miradi hii inalenga kuboresha fursa za upatikanaji wa elimu jumuishi na bora kwa watoto na vijana nchini.

Kwa upande wa UNICEF Tanzania, ujumbe wa shirika hilo uliongozwa na Mkurugenzi wake nchini Tanzania, Bi. Simone Vis, akiwa ameambatana na mtaalamu wa elimu Dkt. Ayoub Kafyulilo pamoja na mhandisi wa miradi ya maendeleo, Bw. Mohamed Hindi. Wadau hao walionesha kuridhishwa na namna TEA inavyosimamia utekelezaji wa miradi, huku wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano endelevu katika kuongeza tija ya uwekezaji wa elimu kwa watoto wa Tanzania.

Dkt. Kipesha aliwashukuru UNICEF kwa kuendelea kuiamini TEA kama msimamizi mkuu wa miradi hiyo muhimu na kuahidi kuwa miradi yote itatekelezwa kwa wakati, kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa. Alisisitiza kuwa utekelezaji mzuri wa miradi hiyo utafungua milango kwa ufadhili zaidi kutoka kwa wadau wa maendeleo na hivyo kuendelea kuinua ubora wa elimu nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!