Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inaendelea kusonga mbele kwa kasi katika kuimarisha na kuboresha miundombinu ya elimu nchini. Lengo la jitihada hizi ni kuhakikisha kila mwanafunzi na mwalimu anapata mazingira bora, salama na rafiki kwa ujifunzaji na ufundishaji.
Kupitia miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, maktaba na maabara za sayansi na nyumba za walimu inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, TEA inawezesha ustawi wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu. Hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha elimu inakuwa chachu ya maendeleo kwa kila mtoto wa Kitanzania.
Wadau wa elimu mna nafasi kubwa kushiriki safari hii ya mageuzi ya elimu kwa kuchangia kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na TEA.
Ili kufanikisha mageuzi haya ya sekta ya elimu hapa nchini, TEA inaendelea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi kutoka ndani na nje ya Tanzania, mashirika ya umma na jamii nzima kuhakikisha kila rasilimali inayowekezwa kwenye Mfuko wa Elimu wa Taifa inaleta tija na matokeo chanya kwenye elimu.