Benki ya Maendeleo TIB imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 408.3 katika miradi ya maendeleo hadi kufikia Desemba 2024 pamoja na mifuko yenye thamani ya shilingi bilioni 222 huku zaidi ya ajira mpya 12,547 zimezalishwa kutokana na benki kufadhili miradi ya maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Bi. Lilian Mbassy
leo Alhamisi Machi 20,2025 Wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 20, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Amesema uwekezaji huu umegusa maeneo ya kipaumbele ya Serikali pamoja na
Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hasa katika Shilingi 162.7 bilioni zimewekezwa
kuongeza usalama wa chakula na kupunguza njaa, Shilingi 4.3 bilioni zimewekezwa
kuboresha elimu kupitia miradi ya taasisi za elimu, Shilingi 22.4 bilioni zimewekezwa
katika upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kupitia miradi ya mamlaka za maji.
Aidha, Benki ya Maendeleo TIB imeripoti kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 630.3 katika miradi ya maendeleo hadi kufikia Desemba 2024. Kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 408.3 zipo kwenye mizania ya Benki, huku mifuko tisa inayosimamiwa na Benki ikichangia uwekezaji
wa Shilingi bilioni 222. Uwekezaji huu ni wamiradi ya muda wa miaka 5-15 katika sekta
mbalimbali za maendeleo.
Mbali na hayo Mbassy amesema uwekezaji mwengine ni Shilingi 11.5 bilioni zimewekezwa katika nishati safi na nafuu kupitia mradi wa upanuzi wa nishati ya umeme vijijini (Tanzania Rural Electrification
Expansion Programme-TREEP), Shilingi 250.7 bilioni zimewekezwa katika ukuaji wa
uchumi na ajira, ikihusisha sekta za utalii, viwanda, na usafirishaji na Shilingi 24.7 bilioni
zimewekezwa kuboresha miji na makazi.
Akizungumzia mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Benki hiyo, Bibi Mbassy
amesema TIB kama benki ya maendeleo ni taasisi ya kisera ambayo ina jukumu la kuunga
mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa hususani kwenye
utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika mwaka 2025 Benki vipaumbele vyake vimejikita katika kuunga mkono juhudi za
Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo,
pamoja na kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema kuwa Benki itaendelea kukuza mtaji wa Benki kwa kushirikiana na taasisi za
fedha za kimataifa ili kupata mikopo ya riba nafuu kwaajili ya kufadhili miradi mikubwa ya
maendeleo yenye athari Chanya kwa jamii na uchumi.