Hali ya uwekezaji nchini Tanzania imeelezwa kuendelea kupata mafanikio makubwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, huku nchi ikisajili miradi mipya 177 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.12 kati ya Januari na Machi 2026.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha ripoti hiyo kwa wanahabari mkoani Dar es Salaam, leo, Alhamisi, Aprili 2, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Gilead Teri amebainisha kuwa miradi hiyo inategemewa kuzalisha ajira mpya 19,750, jambo linalothibitisha kuimarika kwa imani ya wawekezaji nchini.

Sekta ya uzalishaji viwandani imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uwekezaji ikichukua asilimia 51 ya miradi yote, ikifuatiwa na utalii (10%) na majengo ya biashara (10%). Kijiografia, mikoa ya Dar es Salaam (miradi 60) na Pwani (miradi 33) imebaki kuwa vinara wa mikoa iliyoongoza kuvutia uwekezaji kutokana na ubora wa miundombinu ya barabara, umeme, na ukaribu na bandari.
Aidha, kulingana na ripoti hiyo, China imeendelea kushika nafasi ya kwanza kwa kuleta mitaji mingi zaidi (39%) na kuzalisha ajira (60%), ikifuatiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mauritius, na India.
Mradi kielelezo wa Bagamoyo Eco-Maritime City umepata mapokezi makubwa ambapo hadi sasa wawekezaji 48 wameonesha nia ya kuwekeza. TISEZA tayari imesaini mikataba na kampuni tisa (9) zitakazowekeza Shilingi Bilioni 177 katika viwanda vya vifungashio, usindikaji wa korosho, na uunganishaji wa magari (SUV, malori, na mabasi).
Teri amesema kuwa kuna ongezeko la uwekezaji wa wazawa, ambapo Watanzania sasa wanamiliki asilimia 57.06 ya miradi yote (ikijumuisha uwekezaji wa mzawa mmoja mmoja na ubia).

Aidha ameeleza kuwa TISEZA imezindua Kituo cha Huduma Jumuishi (Sourcing and Export Center) katika eneo la BWM SEZ-Mabibo, kikilenga kuwasaidia vijana kati ya 50,000 hadi 100,000 kupata mitaji, vifaa vya kisasa, na masoko ya nje.
Ili kuvutia zaidi uwekezaji, Teri ametangaza mikakati kadhaa ikiwemo kuanzisha vituo vya uwekezaji vya mikoa, kuandaa kitabu cha vivutio vya kodi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kuandaa Kongamano la Uwekezaji la ‘Invest for Impact Tanzania’ litakalofanyika Juni 1, 2026, jijini Arusha.
“Niwaombee Watanzania kuendelea kuboresha na kulinda mazingira ya uwekezaji, kwani, kila nchi duniani imeweka mazingira madhubuti ya kuhakikisha kuna amani na utulivu kwa kuwa na mifumo imara ya kisera, sheria, kanununi na taasisi. umuhimu wa kuboresha na kulinda mazingira ya uwekezaji ni kuendelea kuzalisha ajira, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kuongeza ushindani katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na kusaidia kuwa na bidhaa nyingi zitakazo dhibiti mfumuko wa bei, kukuza uhamishaji wa teknolojia na ujuzi, kupunguza uuagiza wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kukuza sekta mbali mbali”, ameeleza Teri.
Kiujumla, ripoti inaonesha kuwa uwekezaji umekua kwa kasi kutoka miradi 252 mwaka 2021 hadi kufikia miradi 927 mwaka 2025. Mafanikio haya yamechangiwa na utulivu wa kisiasa na sera zinazotabirika, hali iliyosababisha Shirika la Kimataifa la Moody’s kuipa Tanzania daraja la B1 lenye mtazamo thabiti (stable outlook).