Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) limetekeleza agizo la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko kuhusu kuweka samani mbalimbali kwenye kituo cha polisi cha Msimbati kilicho gharimu zaidi ya shilingi milioni 186.
Agizo hilo lilitolewa wakati wa uzinduzi wa kituo hicho cha polisi cha Msimbati alipokuwa kwenye ziara yake aliyoifanya Novemba 17,2024 ambapo Aprili 4,2025 TPDC limekabidhi samani mbalimbali pamoja na vifaa vya tehama kwa ajili ya matumizi ya kituo hicho, zilizogharimu Sh milioni 21.
Akizungumza wakati wa kukabidhi samani hizo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa TPDC Ally Mluge kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo amesema kutokana na kazi ya polisi kuwa na umuhimu kwa jamii hasa kujitoa kwao kwa dhati katika kuhakikisha wanalinda amani na usalama wa raia.
Tpdc wameona ipo haja ya kuunga mkono juhudi zao kwa kuwapa zana zinazohitajika ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni sehemu ya jitihada za tpdc kurudisha kwa jamii zinazolenga kuhakikisha kuwa jeshi la polisi linakuwa na mazingira bora ya kazi.
“Tunatumai kwamba vifaa hivi vitachangia katika kuongeza ufanisi wa kazi zao na pia kuimarisha huduma kwa wananchi.” amesema Ally
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara, SACP Issa Sulemani amekishukuru kituo hicho cha tpdc kwa ujenzi wa kituo cha polisi na kuwanunulia vifaa vya kisasa na amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia maboresho ya jeshi la polisi katika nyanja zote.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amevihakikishia vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuwapa ushirikiano ili waendelee kuwa na mazingira mazuri na rafiki katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Nitoe rai kwa viongozi mbalimbali wa serikali kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama ili waweze kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao za maendeleo katika mazingira rafiki”amesema Sawala
Pia amewataka viongozi hao ikiwemo Wakurugenzi na wakuu wa wilaya ya Mtwara kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutumia sheria na taratibu zote ili kuhakikisha hakuna mtu yoyote anayeweza kuvuruga amani iliyopo katika mkoa huo.
Sambamba na hilo Shirika lisilo la kiserikali la Search For Common Ground linalotekeleza mradi wa Daraja la Amani mkoa wa Mtwara limekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa Jeshi la Uhamiaji katika vituo vya Mtamba Swala na Kilambo mkoani humo.