Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeeleza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari nchini kwa lengo la kukuza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya kodi, hasa matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki (Electronic Tax Stamps – ETS), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupambana na bidhaa bandia, kuongeza mapato ya taifa na kulinda afya za wananchi.
Katika semina iliyowakutanisha wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, siku ya Jumatano Mei 28, 2025 mkoani Dar es Salaam, Kaimu Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Hosea Kidasi, amesema kuwa semina hiyo imelenga kuwawezesha wanahabari kufahamu kwa kina mfumo wa ETS, changamoto zake, mafanikio yaliyopatikana, pamoja na nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha wananchi juu ya ulipaji sahihi wa kodi.
“Tumeona umuhimu wa kuwa na jukwaa mahsusi kwa ajili ya wanahabari ili kuwajengea uelewa wa masuala ya stempu za kielektroniki. Watanzania wengi bado hawafahamu changamoto na fursa zilizopo katika mfumo huu, hali inayochangia kuendelea kuwepo kwa bidhaa bandia sokoni. Kupitia semina hii, tunawawezesha wanahabari kuwa mabalozi wa elimu ya kodi nchini,” amesema Kidasi.
Ameeleza kuwa mfumo wa ETS umeanza kuonesha mafanikio makubwa, ikiwemo ongezeko la makusanyo ya mapato tangu kuanzishwa kwake. Kwa mujibu wa Kidasi, TRA imekuwa ikivuka malengo ya makusanyo ya kodi kwa miezi mfululizo kuanzia Julai 2024 hadi Aprili 2025, jambo linaloashiria mwamko mzuri miongoni mwa walipakodi na utekelezaji wa mifumo madhubuti ya udhibiti.
“TRA inatambua mchango mkubwa wa walipakodi katika maendeleo ya taifa. Mafanikio haya hayawezi kutokea bila ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka na wananchi. Na ndiyo maana tunaona vyombo vya habari kama daraja la muhimu sana katika kusambaza elimu ya kodi kwa umma,” ameongeza Kidasi.
Kwa upande wake, Alfred Mapunda, Meneja Mkuu wa kampuni ya SICPA Tanzania, ambayo ndiyo mtoa huduma wa teknolojia ya ETS kwa TRA, ameeleza kuwa teknolojia ya stempu hizo za kielektroniki ina viwango vya juu vya usalama ambavyo vinaifanya kuwa vigumu kughushi.
“Mfumo wetu wa ETS umejengwa kwa teknolojia ya kisasa inayozuia kabisa kugushi. Tunatumia alama za kiusalama ambazo hazionekani kwa macho ya kawaida, na endapo mtu atajaribu kughushi, inakuwa rahisi sana kubaini bidhaa hiyo. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya bidhaa zenye stempu bandia,” amesema Mapunda.
Paul Walalaze, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi TRA, amesisitiza nafasi ya wanahabari katika kusaidia mamlaka kufikisha elimu ya kodi kwa wananchi, hasa maeneo ya mipakani ambapo bidhaa nyingi kutoka nje huingia na kuna uwezekano mkubwa wa kuuzwa bidhaa zisizo halali.
“Tunataka wanahabari wasaidie kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia programu tumizi ya Hakiki Stempu ili waweze kuhakiki bidhaa kama vile vinywaji au viburudisho kabla ya kuvinywa. Kwa kufanya hivyo, siyo tu kwamba watakuwa wanalinda afya zao, bali pia watakuwa wakishiriki kikamilifu katika kulinda uchumi wa nchi dhidi ya mianya ya ukwepaji kodi,” amesema Walalaze.
Ameongeza kuwa elimu hiyo itasaidia wananchi kuelewa kwanini kodi inalipwa, inatumika vipi, na namna inavyosaidia kuleta maendeleo ya taifa kupitia huduma za jamii kama barabara, shule, hospitali na maji safi.
Kwa upande wa wahariri, Caren-Tausi Mbowe, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akimwakilisha Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile, ameeleza kuwa semina kama hizo ni muhimu, lakini ziongezwe zaidi na ziwe na sehemu ya vitendo kwa wanahabari kutembelea viwandani kuona kwa macho yao namna stempu zinavyowekwa.
“Tunapenda semina hizi ziende sambamba na ziara za viwandani. Tukienda kule na kuzungumza na wazalishaji, tutajua kwa undani changamoto zao, tutaandika habari zenye muktadha na zenye ushawishi. Sisi wahariri tuko tayari kushirikiana na TRA katika kuhakikisha jamii inapata habari za kweli na sahihi kuhusu kodi,” amesema Mbowe.
Aidha, amesisitiza kuwa wanahabari wana jukumu la kuandika habari za maendeleo na kutumia mbinu za uandishi wa habari za utatuzi (Solution Journalism), kwa kueleza wazi faida halisi za ulipaji kodi kwa maendeleo ya Taifa.
“Kazi yetu siyo tu kusema ‘lipa kodi’, bali pia kuwaeleza watu faida zake ni nini. Tunataka watu wajue kwamba kodi yao inajenga shule, barabara, inaboresha afya, na kadhalika. Hapo ndipo wataona thamani ya kushiriki moja kwa moja katika kuiendeleza nchi yao,” ameongeza Mbowe ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF