Latest Posts

TRA YAPONGEZA MCHANGO WA KANISA KATOLIKI KATIKA ULIPAJI WA KODI

Askofu Mkuu Mwandamizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa’ichi, ameahidi ushirikiano wa Kanisa Katoliki na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kuhamasisha ulipaji wa kodi. Askofu Ruwa’ichi amesisitiza kuwa kodi ni msingi wa maendeleo ya nchi na ni wajibu wa kila raia.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, iliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Askofu Ruwa’ichi ameeleza kuridhishwa na juhudi za TRA katika ukusanyaji wa kodi, akisema zinaleta uaminifu na usawa kwa wananchi.

Askofu Ruwa’ichi amesema Kanisa Katoliki litaendelea kutumia nafasi yake kuhimiza ulipaji wa kodi kwa wananchi wake. “Kwa niaba ya Watanzania, niwapongeze TRA kwa kazi kubwa mnayoifanya. Tutajitahidi kuwahimiza watu wazingatie wajibu wao wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa,” alisema.

Pia, ameonesha kufurahishwa na msisitizo wa TRA wa kutenda haki kwa kuhakikisha kuwa kila raia analipa kodi kulingana na uwezo wake bila upendeleo.

Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema lengo la ziara hiyo lilikuwa kumshukuru Askofu Ruwa’ichi kwa mchango wake wa kuhamasisha ulipaji wa kodi, hususan kupitia taasisi za elimu na afya zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki.

“Disemba ni mwezi wa kuwashukuru walipakodi. Tunatambua mchango wa taasisi zenu, hasa katika sekta za elimu na afya, ambazo mara nyingine hunufaika na msamaha wa kodi kulingana na sheria,” amesema Kamishna Mwenda.

Kamishna Mwenda amesisitiza kuwa ulipaji wa kodi ni suala la kiimani na kimaadili kwa kuwa kodi hizo ndizo zinazofanikisha maendeleo katika sekta za elimu, afya, na miundombinu.

“Tunaheshimu taasisi za kidini kwa sababu mna ushawishi mkubwa kwa jamii, na tunaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha kuwa hakuna anayeonewa katika mchakato wa kodi,” ameongeza.

TRA imeahidi kuwasaidia walipakodi ili walipe kodi kwa hiari, huku ikidumisha usawa wa ushindani sokoni. Kwa upande wake, Askofu Ruwa’ichi amehakikisha kuwa Kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana na TRA katika kuimarisha uchumi wa taifa kupitia kodi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!