Baada ya zaidi ya miezi miwili ya maandalizi, Rais wa Marekani, Donald Trump, amezindua rasmi hatua kali za kiuchumi kwa kuzindua vita vya kibiashara dhidi ya mataifa mbalimbali duniani.
Katika hafla iliyofanyika kwenye Bustani ya Rose Garden, Ikulu ya White House, Trump ametangaza Aprili 2 kama “Siku ya Ukombozi” wa Marekani, akisisitiza kuwa hatua hizo zitarejesha ukuu wa uchumi wa taifa hilo.
“Leo ni Siku ya Ukombozi,” Trump amesema. “Tutaifanya Marekani kuwa kubwa na tajiri tena. Nchi yetu imenyang’anywa kwa zaidi ya miaka 50. Hilo halitafanyika tena.”
Kupitia amri ya kiutendaji, Trump ametangaza ushuru mpya wa forodha, ikiwa ni pamoja na 34% kwa bidhaa kutoka Uchina, 20% kwa bidhaa kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU), 24% kwa bidhaa kutoka Japan, 26% kwa bidhaa kutoka India na hadi 50% kwa bidhaa kutoka nchi maskini kama Vietnam na Myanmar huku kiwango cha chini cha ushuru kwa bidhaa zote za nje kikiwa 10%.
Hatua hii inatarajiwa kuathiri biashara ya kimataifa kwa kiasi kikubwa, huku wachumi wakionya kuwa gharama za maisha zitapanda kwa Wamarekani wenyewe kutokana na ongezeko la bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Trump amesema kuwa ushuru huo utaanza kutumika Aprili 5, huku viwango vilivyoongezwa vikianza kutumika Aprili 9. Hata hivyo, ameweka wazi kuwa yuko tayari kwa mazungumzo, akisisitiza kuwa nchi yoyote inayotaka kuepuka ushuru huo italazimika kuondoa ushuru wake kwa bidhaa za Marekani.