Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa Marekani na Iran zitafanya mazungumzo ya moja kwa moja ya ngazi ya juu kuhusu makubaliano ya nyuklia Jumamosi, Aprili 12, 2025, huko Oman. Taarifa hiyo imethibitishwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ambaye amesema mazungumzo hayo ni “fursa kubwa lakini pia mtihani mkubwa” kwa pande zote mbili.
Rais Trump amesema kuwa ikiwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa, basi itakuwa “siku mbaya sana kwa Iran,” akionesha msimamo wake mkali dhidi ya azma ya Iran kumiliki silaha za nyuklia.
Hatua hii imekuja baada ya mvutano wa muda mrefu, ambapo mwezi uliopita Trump alionesha uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi kutokana na kukataliwa kwa pendekezo lake la awali la mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.
Mnamo mwaka 2015, Iran na mataifa yenye nguvu duniani walifikia makubaliano ya kihistoria ya nyuklia (JCPOA), ambapo Iran ilikubali kupunguza shughuli zake za nyuklia na kuruhusu ukaguzi wa kimataifa. Makubaliano hayo yalifanikishwa chini ya utawala wa Rais Barack Obama.
Hata hivyo, mwaka 2016, Rais Trump alijiondoa kwenye makubaliano hayo, akitaka mabadiliko makubwa zaidi. Tangu wakati huo, Iran imekiuka baadhi ya vipengele vya makubaliano hayo na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limeeleza wasiwasi wake kuhusu kiwango cha urani iliyotajirishwa na Iran.
Israel, mshirika wa karibu wa Marekani, imekuwa mstari wa mbele kupinga mpango wa nyuklia wa Iran na imeripotiwa kufikiria mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya taifa hilo kama njia ya kujilinda.
Akizungumza akiwa Ikulu ya White House pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Rais Trump alisisitiza kuwa Iran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia. Kwa upande wake, Netanyahu alisema: “Sisi na Marekani tumeungana katika lengo kwamba Iran isipate silaha za nyuklia kamwe. Ikiwa hili linaweza kufanywa kidiplomasia, kama ilivyofanyika Libya, nadhani hiyo itakuwa hatua nzuri.”
Mazungumzo ya Aprili 12 yanatazamwa kwa makini na jamii ya kimataifa, huku dunia ikisubiri kuona iwapo pande hizo mbili zenye msimamo mkali zitaweza kufikia muafaka au ikiwa hali ya mvutano itaendelea kuelekea machafuko ya kijeshi.