Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa mazungumzo ya kumaliza uvamizi wa Urusi nchini Ukraine “yanaendelea vizuri sana,” lakini akaonya kuwa kuna dirisha dogo la fursa la kufanikisha makubaliano ya kumaliza vita hivyo vya muda mrefu.
Trump ametoa kauli hiyo alipokutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, katika Ikulu ya White House kwa mazungumzo rasmi. Starmer amesisitiza kuwa uongozi wa Marekani utakuwa mhimili wa kudumisha amani nchini Ukraine endapo vita vya miaka mitatu vitamalizika.
“Ikiwa haitatokea haraka, huenda isitokee kabisa,” Trump ameonya, akibainisha kuwa muda wa kufanikisha makubaliano unazidi kuyoyoma.
Kwa upande wake, Starmer alisema: “Umetengeneza fursa kubwa ya kihistoria kufanikisha makubaliano ya amani, makubaliano ambayo nadhani yatashereheshwa nchini Ukraine na duniani kote. Hicho ndicho tunacholenga. Lakini ni lazima tukifanikishe hilo kwa njia sahihi.”
Ziara ya Starmer inakuja baada ya ile ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, aliyefika Washington mapema wiki hii akitoa ombi kama hilo kwa Trump.
Pia, kauli hii inakuja siku moja kabla ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kutembelea Ikulu ya White House kwa mazungumzo na Trump kuhusu mustakabali wa Ukraine.
Wakati huo huo, Trump anaendelea kujiweka kama mhusika mkuu katika juhudi za kusaka amani kati ya Ukraine na Urusi, huku akiweka shinikizo kwa pande zote kuhakikisha mazungumzo haya yanazaa matunda haraka iwezekanavyo.