Wakazi wa Dar Es Salaam wameeleza umuhimu wa amani nchini, Watanzania wakitakiwa kujifunza kutoka kwa mataifa yasiyokuwa na amani namna ambavyo wamekuwa wakipitia changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, Bi Amina Mbegu Rashid, Mkazi wa Dar Es salaam, ameeleza amani ndio msingi wa uhuru wa wananchi kufanya shughuli zao, akisema amani pia imesababisha Taifa kupiga hatua kubwa za maendeleo ambapo bila amani huenda Taifa lisingeshuhudia maendeleo na ustawi uliopo sasa katika nyanja mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa haki za binadamu.
“Amani kwenye Taifa letu ni muhimu sana, imetupa nafasi na uhuru wa kufanya mambo yetu bila shuruti. Kwenye nchi za wenzetu kuna shida nyingi sana ambapo hata kutembea tu imekuwa changamoto, hapa kwetu hakuna mwenye viroba 20 ama 30 ndani vya chakula kwahiyo amani ikitoweka unaweza kuona changamoto ambayo tutaipitia hasa katika upatikanaji wa huduma muhimu ikiwemo za matibabu kwahiyo amani ni kitu muhimu sana.” Amesisitiza Bi Amina Mbegu.
Kulingana na wachambuzi mbalimbali wa siasa na maendeleo, wameeleza kuwa amani ni msingi mkuu wa maendeleo, ustawi wa jamii, na utulivu wa kisaikolojia, ikiruhusu shughuli za kiuchumi, elimu, na maisha ya kila siku kustawi bila hofu ya vurugu au migogoro. Inajenga heshima, uvumilivu, na maelewano kati ya watu, huku ikipunguza ushawishi wa vikundi vya kigaidi na chuki.
