Na Josea Sinkala, Songwe.
Tume huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC), imefungua mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi mkoani Songwe na kukutanisha wadau mbalimbali wa uchaguzi.
Miongoni mwa makundi yaliyoshiriki kwenye mkutano huo ni waandishi wa habari na wahariri, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, viongozi wa mkoa, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi kutoka asasi za kiraia.
Akitoa hotuba ya mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) jaji wa Mahakama ya rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele, mkurugenzi wa usimamizi wa uchaguzi Grayson Orcado, amesema;
“Kufanikiwa kwa zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura kwa mkoa wa Songwe kunategemea sana ushiriki wenu (wadau wa uchaguzi) katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wenye sifa wajitokeze kwa wingi kuandikishwa na kuhamasisha au kuboresha taarifa zao. Ni matarajio ya tume kuwa mtakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuwahamasisha wananchi ili zoezi hili lifanyike kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa”, amesema Grayson Orcado kwa niaba ya mwenyekiti wa Tume jaji Mwambegele.
Naye Saida Hilal Mohamed ambaye ni kaimu mkurugenzi wa uchaguzi (mkurugenzi wa idara ya uchaguzi), amewataka wadau hao wa uchaguzi kwenda kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.
“Kuandikishwa ni raia yeyote wa Tanzania aliyefikisha miaka 18 au atakayefikisha umri huo hadi Oktoba 2025 lakini kwa aliyehama kutoka eneo moja kwenda lingine vilevile ni fursa kwa watu waliobadili hadhi zao na wangependa zionekane kwenye vitambulisho vyao labda Saida Hilal nikaamua kuolewa nataka jina la bwana lionekane, wengine kuna watu wamepata udaktari hivyo tuwahimize wajitokeze kujiandikisha au kupatiwa kadi mpya na ni zoezi la muda mfupi ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wasio na sifa kwenye daftari”, amesema Saida Mohamed.
Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wamesema wapo tayari kwenda kuhimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuhuisha taarifa zao kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tume huru ya Taifa ya uchaguzi ndio inasimamia zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la mpiga kura na uandikishaji wapiga kura wapya zoezi linalotarajiwa kuanza Januari 12 hadi Januari 18, 2024 ambapo litafanyika katika mikoa wa Songwe, Rukwa, Njombe na Halmashauri kadhaa za mkoa wa Ruvuma.