Na Josea Sinkala, Mbozi Songwe.
Mbunge wa zamani wa jimbo la Mbozi mkoani Songwe (CHADEMA) Pascal Yohana Haonga, amesema Chama chake (CHADEMA) kitafanikiwa kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kupitia ushawishi wao kwa wananchi kuhakikisha uchaguzi huo haufanyiki kwa vyama vyote.
Haonga amesema hayo wakati akizungumza jimboni kwake Mbozi mkoani Songwe alipohojiwa kuhusu namna wanavyotekeleza kampeni yao ya No reforms no election na ikiwa watafanikiwa.
Amesema Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendelea na mikutano ya hadhara kote nchini kuelimisha wananchi kupata uelewa wa sheria zihusuzo masuala ya uchaguzi ambazo zinaelezwa kuwa sio rafiki kwani zimejaa upendeleo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwabana wapinzani na kudai upinzani unapigania upatikanaji wa sheria nzuri za kusimamia chaguzi ili wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
Pascal Haonga ambaye alikuwa Mbunge wa jimbo la Mbozi kwa kipindi cha mwaka 2015-2020, ameeleza kuwa wanaopinga au kubeza kampeni ya No reforms no election huenda wakawa na manufaa ya mfumo wa sasa wa uchaguzi anaodai unainufaisha CCM na kuwataka wananchi kuiunga mkono CHADEMA kuhakikisha Serikali inafanya marekebisho ya sheria na kanuni za uchaguzi ikiwemo kushughulikia tume huru ya uchaguzi ambayo viongozi na wajumbe wake hawatokani na Chama tawala.
Pamoja na hayo, kada huyo wa upinzani ameeleza kusikitishwa kwake na matukio ya utekaji, kupotea kwa baadhi ya wananchi na mengineyo ambapo amesema uongozi wa Serikali ya awamu ya sita haina tofauti na Serikali ya awamu ya tano ikiwemo kwenye uwekaji mazingira magumu ya kisiasa hususani kwa vyama vya upinzani.
Amesema mabadiliko ya sheria za uchaguzi yasipofanyika basi watahakikisha wanazuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu baadaye Oktoba 2025.